Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete juzi amekutana na mtoto wa Kitanzania ambaye ni Bingwa wa
Dunia wa mchezo wa kuruka kamba, Hamisi Kondo mwenye umri wa miaka 14.Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Ikulu, mbali na kukutana na Rais, Kondo na wenzake pia walifanya
maonesho ya mchezo huo kwa Kikwete ambaye amefurahishwa na vipaji vya watoto
hao wa Kitanzania
.Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kikwete
amekutana, na Kondo pamoja na washiriki wengine waliounda timu ya Tanzania
iliyoshiriki katika Michuano ya Dunia ya Kuruka Kamba iliyofanyika Florida,
Marekani kati ya Julai 5 hadi 13, mwaka huu ambapo nchi 14 zilishiriki.Mbali na Tanzania, nchi nyingine
zilizowakilisha Bara la Afrika katika mashindano hayo ni Afrika Kusini na
Kenya. Miongoni mwa nchi nyingine duniani ziliwania medali katika michuano hiyo
ya Dunia ni Marekani yenyewe, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Mexico na Japan.
Kondo, ambaye alilelewa kwa muda katika
Kituo cha Watoto Yatima cha Dogo Dogo Center cha Dar es Salaam, sasa anasoma
katika Shule ya Msingi ya Seaside Catholic School, mjini Seattle, Jimbo la
Washington ambako mwezi ujao anatarajiwa kuingia darasa la saba.
Mtoto huyo ambaye anaondoka nchini leo
kurejea Marekani, aliondoka nchini mwaka jana baada ya kuwa ameonesha kipaji
kikubwa katika mchezo wa kuruka kamba.
Kabla ya kwenda Marekani alikuwa ameshinda
ubingwa wa Tanzania na ule wa Afrika Mashariki katika mashindano yaliyofanyika
mwaka 2010 mjini Mombasa, Kenya.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba kwenye ujumbe
huo uliokutana na Rais Kikwete, alikuwepo pia Mama Amy Kennedy ambaye yeye
pamoja na mume wake, Dennis Kennedy ndiyo wafadhili wakuu wa Kondo na
wanamiliki moja ya sehemu bora zaidi za kufanyia mazoezi duniani.
"Ni wafadhili hao waliomtafutia Kondo
shule kule Marekani na wanaendelea kulipia gharama za masomo yake, kugharamia
mazoezi yake, kulipia gharama zake za usafiri kwenda kwenye mashindano
mbalimbali," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Wafadhili hao ndiyo waliisafirisha timu ya
Tanzania, kwenda kushiriki katika mashindano hayo ya Marekani ambako pia
walilipia chakula na malazi ya timu hiyo.
No comments:
Post a Comment