29 August 2013

WATUMISHI WA UMMA KUSHUGHULIKIWA



 Na Yusuph Mussa, Lushoto
MK U U w a Wi l a y a y a Lu s h o t o , Al h a j j M a j i d M w a n g a amesema ataendelea kuwashughulikia watendaji wa kata na vijiji wanaodharau utawala wake kwa kusema kwa sasa Jimbo la Bumbuli halina Mkuu wa Wilaya hivyo kukataa kutii maagizo yake.

Akizungumza juzi kwenye warsha ya siku mbili kwa watendaji wa vijiji na kata wa Halmashauri mpya ya Bumbuli ili kufundishwa majukumu yao, aliwaasa watendaji hao kuwa pamoja na Bumbuli kupata halmashauri mpya, bado ipo chini ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto.
"Kuna watendaji wa kata kama wanne hivi nimesikia wanasema baada ya kupata halmashauri sasa wanasubiri Mkuu wa Wilaya yao na kudharau maagizo yangu. Nasema watendaji hao wanajidanganya kilichopatikana ni halmashauri, lakini Mkuu wa Wilaya bado ni mmoja.
"Na hilo si ajabu, Moshi kuna Manispaa na Halmashauri ya Moshi Vijijini, na Arumeru ni vivyo hivyo. Si mnasema mimi ni mzee wa kuweka watendaji ndani, basi endeleeni kusema mimi si Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Bumbuli, lakini mtakiona kile ninachosema," alisema Mwanga.
Mwanga alisema kata nyingi ofisi zao zinafungwa muda wa kazi, huku baadhi ya watendaji wanaondoka maeneo ya kazi na kuwaachia watoto na ndugu zao kukaimu matokeo yake siri za Serikali zinakutwa zimesambaa mitaani.
"Itabidi tuwaite mashekhe na wachungaji wawaombee watendaji hawa kwa kushindwa kuwajibika. Nilitumia usafiri wa binafsi na kukuta kata nane zimefungwa na watendaji hawapo kazini, sijui tutafute shekhe na mchungaji awaombee viongozi hawa.
"Lakini wamekuwa na tabia ya kuondoka eneo la kazi na kuwaachia ofisi watoto na ndugu zao wanakaimu, kesho yake utakuta nyaraka za siri za Serikali zipo mitaani. Lakini utakuta vikao havifanyiki, lakini wanaghushi mihutasari kuonesha kuna watu wamehudhuria, tena kikao hicho utakuta ni cha kutoa fedha," alisema Mwanga.
Mwanga alisema anafahamu kuwa baadhi ya watendaji wanakaimu zaidi ya miezi kumi bila kulipwa mshahara wala posho, lakini hicho kisiwe kigezo cha kuwafanya kucheza mchezo mchafu na kuiba fedha za miradi ya wananchi inayopelekwa kwenye kata na vijiji vyao na kuamini halmashauri italipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatrice Mshomisi alisema maudhui ya warsha hiyo ni kuwakutanisha watendaji hao ili waelewe majukumu yao, lakini pia waeleze changamoto wanazokutana nazo sehemu za kazi.
Hivi karibuni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Vuga, Ali Shenkawa aliwekwa ndani na Mkuu wa Wilaya baada ya kudaiwa kupuuza agizo la kuwaeleza viongozi wa vijiji ambao ni Mwenyekiti na Mtendaji kila kijiji washiriki kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Tarafa.

No comments:

Post a Comment