20 August 2013

WANAFUNZI WA UDAKTARI WALILIA RUZUKU



 Na Martha Fataely, Hai
BAADHI ya wanafunzi wa udaktari na uuguzi katika Chuo cha Machame wilayani Hai, wanashindwa kumaliza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya Serikali kutotekeleza ahadi yake ya kukipatia ruzuku chuo hicho ili kujiendesha.

Rais wa wanafunzi wa chuo hicho, John Ware alisema kutotekelezwa kwa ahadi hiyo kunawaathiri kwa kiasi kikubwa na kuwafanya baadhi ya wanafunzi kushindwa kumaliza masomo yao kwa ukosefu wa gharama za kujitegemea.
Waganga 50 na wauguzi 36 waliomaliza mafunzo ya miaka mitatu ya fani hizo wamekumbusha ahadi hiyo katika risala yao wakati wa mahafali ya 42 ya waganga hao, mahafali ya kwanza ya wauguzi katika chuo hicho na uzinduzi wa ukumbi wa mikutano na bwalo la chakula la chuo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa chuo hicho, Dkt. Elifinya Massawe ameiomba Serikali iongeze idadi ya watumishi wa hospitali na walimu wa chuo hicho ili ihudumie wananchi na kutoa wataalamu wengi watakaokidhi mahitaji ya Serikali ya kuwahudumia wananchi vijijini.
"Hii ada inayolipwa na wanafunzi ndiyo tunaitumia kwa ajili ya kulipa mishahara na shughuli nyingine muhimu, miaka mitatu sasa Serikali haijatupatia ruzuku, kutokana na hilo ada ni kubwa, wanafunzi 2 wa Tanzania na Wakenya watatu walikatisha masomo yao mwaka jana," alisema.
Akibariki wahitimu ukumbi na bwalo hilo Askofu Dkt. Martin Shao wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini inayomiliki chuo hicho amewataka waganga na wauguzi hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa bila kutanguliza masilahi yao.
"Nyinyi mnamaliza leo, mnakwenda kulitumikia taifa ni vyema mkatanguliza masilahi ya taifa kuliko yenu binafsi, kumbukeni viapo vyenu," alisema.
Mapema Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwanri aliwataka wataalamu wa fani mbalimbali kuacha uchakachuaji wa taaluma zao ili kuepusha taifa kupata madhara.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mwanri, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt. Ibrahim Msengi alisema kitendo cha kuchakachua taaluma kutasababisha taifa kupata hasara kwani wataalamu hao bandia hawana uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi au kuleta mabadiliko.

No comments:

Post a Comment