06 August 2013

WAKULIMA WAVIMBIA SERIKALI


Esther Macha, Mbeya na Said Hauni, Lindi
WAKATI Sikukuu ya Wakulima ya Nanenane ikiwa imekaribia kufikia kileleni, kumeibuka mgongano baina ya Chama cha Wakulima (TASO) na Serikali kuhusu siku ya kufanyika kwa maadhimisho hayo kati Agosti 7 na 8, mwaka huu
.Mgongano huo umekuja baada ya Serikali kutaka maadhimisho hayo yafanyike Agosti 7, mwaka huu TASO kikiweka msimamo wake wa kusherehekea maadhimisho hayo Agosti 8, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa TASO, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kapteni Mstaafu Noel Nkoswe, wakati wa mkutano wa majumuisho na waandishi wa habari baada ya kuibuka vuta nikuvute na serikali kuhusu kilele cha maadhimisho hayo ya wakulima.
Kapteni Nkoswe, alisema wao kama chama cha wakulima msimamo wao upo pale pale, ni sherehe hizo zifanyike Agosti 8, mwaka huu kama ilivyopangwa kila mwaka.
"Wa k u l ima we t u l a z ima washerehekee sikukuu yao kama kawaida mpango wa kubadilisha siku haupo kabisa. TASA tunafanya maadhimisho Agosti 8 na zawadi za wakulima tutatoa siku hiyo hiyo na wao kama serikali watafanya kiserikali kama kawaida, sisi upande wetu sikukuu yetu ni Agosti 8," alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, alisema wamepokea barua ya Serikali inayotaarifu kilele cha Nanenane ni Agosti 7, mwaka huu kutokana na Sikukuu ya Idd kuaangukia Agosti 8, mwaka huu.
"Sisi serikali tunafanya maadhimisho haya Agosti 7 mwaka huu kama barua ya serikali ilivyoagiza kuwa kilele hicho kifanyike," alisema.
Wakati huo huo, wakulima Kanda ya Kusini, inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, wametakiwa kuacha tabia ya kilimo cha mazoea, badala yake wakigeuze kuwa cha kibiashara kwa kuzalisha zaidi mazao yanayolenga mahitaji halisi ya walaji.
Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa TASO Kanda ya Mtwara, Menas Likuku, alipokuwa akisoma risala, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane,yanayofanyika viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi.
Akisoma risala hiyo mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia, mwenyekiti huyo wa TASA alisisitiza wananchi kuzalisha mazao kwa malengo ya kibiashara na kuangalia fursa za masoko yaliyopo.
Likuku alisema TASA kanda ya kusini inawahamasisha wakulima wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa lengo la kukuza ustawi wa jamii kupitia uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na sekta nyingine.
Alizitaja sekta hizo kuwa ni pamoja na uvuvi, urinaji wa asali, viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa kulenga masoko yaliyopo na yale yanayotarajiwa kuwepo kutokana na kukua kwa sekta ya gesi.
Mwenyekiti huyo alisema tangu kuanzishwa kwa maonesho ya hayo miaka 10 iliyopita, kumekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja kukamilika kwa upimaji wa viwanja (50) vya eneo la ndani ya kwa ajili ya wadau.

No comments:

Post a Comment