NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Aggrey Mwanri ameagiza watoto wote kwenye shule za msingi ni lazima waende
shule.Alisema hata kama hawana fedha za michango ama sare waruhusiwe kuvaa
nguo za kawaida huku akiagiza suala la michango ni la wazazi sio wanafunzi.
Aliyasema hayo juzi wakati anahutubia wananchi kwenye mji wa Chanika
uliopo Halmashauri ya Mji Handeni ambapo alisema kitendo cha kuwarudisha watoto
nyumbani kutokana na michango mbalimbali kuna baadhi ya wazazi wanafurahia hasa
wenye watoto wa kike.
"Watoto waende shuleni hata kama wamevaa pensi nyanya. Na pia
kutokutoa ada au michango sio suala la mtoto bali mzazi. Hivyo vita ya kudai
michango ifanywe kwa wazazi walioshindwa kulipa michango hiyo.
"Kitendo
cha kumrudisha mtoto nyumbani akikutana na wazazi wasiopenda watoto wao kusoma
na kama ni mtoto wa kike, atafurahia kwa vile atakuwa amepata binti wa
kuozesha. Au nyinyi hamjasikia kuna wazazi wanawalaumu watoto wao waliofaulu.
Mzazi anamwambia mtoto si unaona nilikwambia usifanye vizuri, unaona sasa umefaulu,"
alisema Mwanri.
Akizungumza
kwenye mkutano wa majumuisho baada ya ziara ya siku mbili kwenye Halmashauri ya
Wilaya na ile ya Mji wa Handeni, Mwanri aliwataka watumishi kuwasikiliza
wananchi na kumaliza kero zao badala ya kuwachenga na kwenda kunywa supu ama
kubishana mambo ya mpira.
"Hakuna
kitu kinawakera wananchi kama kutosikilizwa matatizo yao...wewe muda wote upo
kwenye 'Pub' unapiga supu, ukifika ofisini unabishana mambo ya Simba na
Yanga," alisema Mwanri.
Mwanri ameagiza
majengo yote ya Serikali yanayojengwa nchini yawe na mifumo ya maji na umeme ni
baada ya kukuta baadhi ya majengo kwenye Wilaya ya Handeni yakiwa hayana mifumo
hiyo na kusema majengo hayo ikiwemo zahanati na nyumba za walimu haziwezi kukaa
milele bila kuwekwa umeme.
Akisoma
taarifa, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Thomas Mzinga alisema
halmashauri yao ambayo ni mpya inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo
miundombinu ya maji na uchakavu wa mitambo kwenye Mji wa Handeni na kuungua
mara kwa mara kwa mota za pampu za kusukuma maji.
"Pia tuna uhaba wa
ofisi kwa baadhi ya maofisa kama vile mwanasheria, idara ya elimu na sekondari,
maji, ardhi, maliasili na mazingira na ofisa manunuzi, uhaba wa fenicha elimu
ya msingi na sekondari, afya, huku tukiwa hatuna ukumbi wa mikutano, uhaba wa
usafiri na vitendea kazi. Na Halmashauri ya Mji iliomba fedha za kujenga ofisi
kuu lakini ombi halikupita," alisema Mzinga
No comments:
Post a Comment