28 August 2013

WAKAZI KAGERA KUKOSA UMEME KWA WIKI 40



Na Livinus Feruzi, Bukoba
MATENGENEZO ya uboreshaji njia kuu za kusafirisha umeme yanayotarajiwa kufanywa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kutoka Masaka nchini Uganda hadi Mutukula nchini Tanzania, yatasababisha Wilaya tatu za Mkoa wa Kagera kukosa huduma ya umeme kwa wiki 40.

Wilaya ambazo zitaathirika na uboreshaji huo ni pamoja na Bukoba, Muleba na Karagwe, ambapo Meneja wa TANESCO, mkoani humo, Martin Madulu, alisema zaidi ya kilomita 1,000 za njia ya umeme zitafanyiwa ukarabati.Alisema matengenezo hayo yataanza Septemba mosi mwaka huu na yatafanyika kwa siku tatu kila wiki kwa majuma 40.
"Umeme utakuwa ukikatwa siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuanzia asubuhi hadi jioni... hali hii inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka maeneo husika."Viongozi wa pande zote (Uganda na Tanzania), wamekubaliana kufanya ukarabati huu ili kuboresha huduma...mapendekezo ya viongozi wa Uganda walitaka umeme ukatwe wiki nzima ili matengenezo haya yachukue miezi mitano," alisema.
Aliongeza kuwa, pendekezo hilo halikukubaliwa baada ya kubainika kuwa, madhara yangekuwa makubwa miongoni mwa jamii. Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu kwa muda wote wa matengenezo hayo

No comments:

Post a Comment