16 August 2013

WAHAMIAJI 8509 WAREJEA MAKWAO



Na Mwandishi Wetu
WAHAMIAJI haramu 8,509 kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda, wameondoka nchini kwa hiari yao baada ya agizo la Rais Jakaya Kikwete, ambalo alilitoa hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Kagera.Wahamiaji hao, wametoka katika Mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma ambapo taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ilisema kati ya wahamiaji hao, 5,521 wamerudi nchini Rwanda, Burundi 2,744 na Uganda 244.

Katika operesheni hiyo, silaha 60 zimerejeshwa kwa hiari zikiwemo bunduki aina ya SMG na magobole ambapo taarifa hiyo iliongeza kuwa, operesheni ya kuwarejesha wahamiaji hao pia imehusisha urejeshaji wa mali na mizigo.Vitu vingine vilivyorejeshwa ni mifugo 1,996 katika nchi hizo. Kurejea kwa wahamiaji hao ni utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete ambaye alitoa siku 14 wawe wameondoka nchini kwa hiari yao ndani ya kipindi hicho.
"Serikali imefurahishwa sana na ushirikiano tuliopata kutoka nchi za Rwanda, Burundi na Uganda hasa za kuwapokea hawa wahamiaji wakishirikiana na nchi yetu katika kazi hii."Tunawaomba wahamiaji wengine ambao bado wako nchini, waondoke haraka iwezekanavyo kabla hatua ya kuwaondoa kwa nguvu hazijaanza," iliongeza taarifa hiyo

No comments:

Post a Comment