16 August 2013

SUMAYE AKOSOA VIPENGELE RASIMU YA KATIBANa Darlin Said
WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, amesema Rasimu ya Katiba Mpya imeshindwa kuonesha msisitizo wa kutatua matatizo ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya ambayo husababisha Watanzania wakose imani na Serikali yao.Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Katiba la Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), ambao ulijadili Rasimu ya Katiba Mpya
.Alisema bila kuyadhibiti madhambi hayo katika nchi, Katiba hata iwe nzuri kiasi gani itakuwa kazi bure ambapo wananchi hawataona manufaa ya katiba hiyo, matunda ya juhudi zao.Aliongeza kuwa, ingawa rasimu hiyo ni nzuri ila bado haijagusa mambo hayo ambayo yanawatesa watu kama rushwa ambayo inahatarisha amani ya nchi.
"Kulingana na ukubwa wa matatizo haya kwa amani ya nchi na ukuaji wa uchumi, natamani rasimu hii ingetaja kipengele cha kuundwa Mahakama Maalumu ya makosa hayo na iruhusu adhabu kali kwa wahusika," alisema Bw. SumayeAkizungumzia ufisadi, Bw. Sumaye alisema tatizo hilo ni kubwa ambalo linahujumu uchumi wa nchi hivyo kuwakatisha tamaa wananchi kutokana na ongezeko la ugumu wa maisha.
Alisema tatizo la dawa za kulevya, pamoja na kuwaathiri zaidi vijana, pia linasababisha kushusha heshima ya Tanzania na kuvitaja vipengele alivyodai vina utata likiwemo suala la Muungano."Ni vyema tukaainisha changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa Serikali mbili na kuzipatia ufumbuzi wake...kama tutashindwa kupata ufumbuzi, mivutano hiyo itaendelea kuwepo katika Serikali tatu na zitatokea changamoto nyingine hasa katika Serikali ya Muungano na ile ya Tanganyika," alisema.
Aliyataja maeneo mengine yanayopaswa kujadiliwa kuwa ni suala la Makamu wa Rais kushika madaraka kama rais atafariki na kudai kuwa, huo ni mfumo mbovu kwa sababu rais lazima achaguliwe na kama atakufa kutasababisha minong'ono hata kama Makamu wa Rais hausiki na kifo chake.
"Rasimu haielewi uwiano utakuwa wa namna gani, kama hakutakuwa na ufafanuzi kunaweza kutokea usumbufu katika Muungano...eneo lingine ni lile la mapato lazima ielezwe wazi," alisema Bw. Sumaye.
Madaraka ya Rais
Bw. Sumaye alisema, kuna maeneo mengine ambayo watu wameyatolea maoni hasa suala la madaraka ya rais jambo ambalo hata yeye anaamini baadhi ya nafasi anazoteua kiongozi wa nchi zinapaswa kuthibitishwa na vyombo vingine kama Bunge au chombo kingine kwa mujibu wa katiba husika.
Alisema hiyo haimpunguzii rais madaraka bali inamsaidia na kumkinga. "Jambo hili linafanyika katika nchi nyingi sioni kwanini liwe na shida kwetu hivyo liangaliwe," alisema.
Naye kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Kingunge Ngombalemwilu, aliwataka viongozi kuwa waadilifu na wafuate sheria ili kuepusha matatizo yanayoibuka hivi sasa na kujenga maisha ya wananchi.
.
.

No comments:

Post a Comment