30 August 2013

WAFUNGWA WARUHUSIWE TENDO LA NDOA KATIBA MPYANa Yusuph Mussa, Korogwe
BAADHI ya wadau wa masuala ya jinsia wamependekeza kuwa ili kukabiliana na masuala ya ushoga na usagaji, Katiba Mpya iruhusu wafungwa kukutana kimwili na wenza wao, kwani vitendo hivyo chanzo chake ni gerezani hasa kwa vijana wanaokula 'unga' na kuvuta bangi.

Hayo yalisemwa juzi kwenye kikao cha maboresho ya Rasimu ya Katiba Mpya, kilichofanyika siku tatu kwenye Kijiji cha Makaburini kwa kuratibiwa na asasi ya Tanzania Environment Relatives Organization (TERO) ya mjini Korogwe kwa ufadhili ya Shirika la The Foundation for Civil Society la jijini Dar es Salaam.
"Mfungwa akubaliwe kukutana kimwili na mume au mke wake. Kitendo cha kuwakatalia wafungwa kukutana kimwili na wake au waume zao kunachochea vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia moja na vijana wengi wameharibikia gerezani na kujikuta vitendo hivyo vinaingia mitaani" alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerenge- Makaburini Mohamed Mdoe.
Mdoe alisema ili kuimarisha ulinzi na usalama mabalozi wawe viongozi wa Serikali badala ya chama, kwani kutokana na vitongoji kuwa vikubwa, Mwenyekiti wa Kitongoji hana uwezo wa kuratibu watu wote walioingia kwenye kitongoji chake, lakini balozi ana uwezo kutokana na eneo lake kuwa dogo.
Naye Mwalimu Mkuum, Shule ya Msingi Makumba, Sisili Mhina alisema hakuna sababu ya kuwafunga watu waliotukanana ama kuiba vitu vidogo vidogo, huku ni kujaza magereza na kuliongezea Taifa mzigo na kudai suluhu ya watu hao ni kufungwa kifungo cha nje wakiwa wanaitumikia jamii.
Naye Hamisi Mijuza alisema vyeti vya kuzaliwa visitolewe kwenye Ofisi ya Mkuu wa wilaya bali kwenye ofisi za vijiji na kata kwani hao ndio wanaowajua watoto na wazazi wao kwao ni wapi na kudai wanapokwenda kwa Mkuu wa Wilaya wanapoteza muda mwingi na gharama bila sababu za msingi.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Kata ya Kerenge, Stephen Daffa alisema Serikali kuogopa kukosolewa na waandishi wa habari katika masuala ya kitaifa ni sawa na kukimbia kivuli chake, kwani katika nchi zilizoendelea vyombo vya habari ni mhimili wa nne, na unasaidia Serikali kujua wapi inakwenda vizuri na wapi inakosea.
"Serikali isiingilie vyombo vya habari kwa vile vinasaidia kuelimisha umma. Lakini hapo hapo vinakosoa na kuona mambo yanakwenda vizuri, hivyo kujaribu kuvibana ili visifanye kazi zake vizuri ni kuchelewesha maendeleo ya wananchi," alisema Mchungaji Daffa.  

1 comment:

  1. IKUMBUKWE JELA NI CHUO CHA MAFUNZO JE TUNAWAHAMASISHA WAHALIFU KUFURAHIA KUYARUDIA MAKOSA SI RAHISI KUJUTA NA KUACHA UOVU

    ReplyDelete