30 August 2013

MATATANI AKITUHUMIWA KUMUUA MUMEWENa Abdallah Amiri, Igunga
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora jana lilimfikisha mahakamani, Msua Malanda (37), mkazi wa kijiji cha Segerei, Kata ya Igoweko wilayani Igunga kwa kosa la kumpiga mumewe chupa kichwani na kusababisha kifo chake.

Akisomewa shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga, Ajali Milanzi, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Dezidery Kaigwa, aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kusababishia kifo.
Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 196 (A) kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambapo inazuia kufanya makosa kama hayo.
Aliiambia mahakama kuwa Agosti 24, mwaka huu saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Segerei kata ya Igoweko wilayani hapa mshtakiwa alimpiga chupa kichwani mume wake, Abdallah Hamisi (48) na kumsababishia kifo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.Mshtakiwa alirudishwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 13, mwaka huu, itakapotajwa tena

No comments:

Post a Comment