05 August 2013

WAFANYAKAZI TAZARA KUTINGA KWA PINDA


 Na Heri Shaaban
WAFANYAKAZI wa Shirika la Reli la Tanzania na Zamb i a (TAZARA) wamepanga kuandamana kwenda Ofisi za Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufikisha kilio chao baada ya kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu bila kulipwa mishahara yao
.Hatua ya kupanga maandamano ya kwenda kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupeleka kilio chao inafuatia mawaziri karibu wanne waliokaa katika Wizara ya Uchukuzi akiwemo Harrison Mwakyembe kushindwa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wafanyakazi wa TAZARA na Uongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Katibu wa Wafanyakazi Kanda ya Dar es Salaam TAZARA na TRL (TRAWU) Erias Chizingwa alisema kesho Jumatatu watakutana katika kikao cha TRAWU baada ya kikao cha mwishoni mwa wiki kushindwa kutoa majibu.
Chizigwa alisema wamepanga kukutana Agosti 5, mwaka huu katika kikao chao ili kutoa maamuzi ya kupeleka kilio chao kwa Mizengo Pinda ili aweze kushughulikia malalamiko yao ya kucheleweshewa mishahara toka mwezi Mei hadi sasa.
"Mimi sio msemaji lakini, tunataka kufanya maamuzi hayo katika kikao chetu cha pamoja wafanyakazi wote wa TAZARA kwenda kwa Pinda au aje kusikiliza kilio chetu na kutolea ufumbuzi baada ya mawaziri zaidi ya wanne waliokuwepo awali na sasa hivi, katika Wizara ya Uchukuzi kushindwa kushughulikia matatizo ya mishahara na changamoto zinazotukabili kama wafanyakazi.
Alisikitishwa na Jeshi la Polisi kuingilia kuvuruga mkutano wao wa Agosti 2, mwaka huu pamoja na kupora kamera ya mwandishi wa Kituo cha Chanel Ten Elia Ruzika na kumfunga pingu, wakidai mkutano huo sio halali ulioandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Njia ya Reli TRAWU wakati ulifuata taratibu zote na kupewa kibali.
Wa k a t i h u o h u o , Ka t i b u wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Mwakalinga amelionya Jeshi la Polisi kuacha kuingilia kati kinyume cha taratibu ya mafunzo yao.
Mwakalinga ametoa tamko hilo kutokana na kusikitishwa na mwenendo wa kazi wanazofanya Jeshi la Polisi kuvuruga mikutano ya wafanyakazi wakati wakidai maslahi kazini ili waweze kupata haki zao.
"Jeshi la Polisi kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao sio kuvuruga mikutano au kupiga raia wakati wakidai haki kama walivyopora vifaa vya mwandishi wa Chanel Ten na kumfunga pingu, kwani kila mtu ana uhuru wa kutumia na kutoa mawazo yao hadharani kama katiba inavyoruhusu,"alisema Mwakalinga.
Alisema utaratibu waliotumia wafanyakazi TAZARA ni mzuri wa kuomba kibali na kukutana, sio kama wafanyakazi wa nchi za wenzetu wanatumia nafasi yakupeleka kilio chao kwa maandamano barabarani.
Alisema kama polisi wanatumwa na Serikali alishauri polisi wajiunge na vyama vya wafanyakazi waweze kufundishwa sheria za kazi kwa ajili ya kulinda, kutetea na kudumisha mauhusiano ya kazi.

1 comment:

  1. Mungu walaani wote waliochagia TAZARA kushindwa kujiendesha kifaida ni mafisadi hao Mungu waangamize jehanamu wakimaliza maisha yao hapa duniani amina

    ReplyDelete