Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAI S wa Za n z
i b a r n a Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein
amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali anayoiongoza ni kuhakikisha huduma muhimu
za afya zikiwemo kinga na tiba zinapatikana kwa urahisi kwa wananchi wote.
Akizungumza na
Rais Mstaafu wa Marekani, Bill Clinton ofisini kwake Ikulu jana, Dkt. Shein
alisema Zanzibar imepiga hatua katika utoaji huduma za kinga na tiba kwa
wananchi wake lakini changamoto inayokabiliana nayo ni namna ya kuyafanya
mafanikio hayo kuwa endelevu.
"Tumepata
mafanikio katika kinga na tiba kama vile malaria na vifo vya watoto wachanga
lakini changamoto inayotukabili ni mafanikio haya kuwa endelevu," alieleza
Dkt. Shein.
Hata hivyo Rais
alibainisha kuwa pamoja na kujivunia mafanikio hayo anatambua kuwa mafanikio
hayo ni matokeo ya jitihada za pamoja kati ya Serikali na washirika wake wa
maendeleo ukiwemo Mpango wa Upatikanaji Huduma za Afya wa Clinton (Clinton
Health Access Initiative-CHAI) ulio chini ya Taasisi ya Clinton (Clinton
Foundation).
"Baadhi ya
wenzetu (nchi nyingine) huja kujifunza kujua tumepata vipi mafanikio haya
lakini sisi tunatambua kuwa ni matokeo ya jitihada za pamoja na washirika wetu
mkiwemo nyinyi (Clinton Foundation) hivyo hatuna budi kueleza shukrani zetu
kwenu kwa kutuunga mkono," alisema Dkt. Shein.
Aliipongeza
taasisi hiyo kwa jitihada zake za kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya
kwa nchini zinazoendelea ambapo kwa Zanzibar taasisi hiyo imekuwa ikisaidia
katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa, huduma kwa watu wenye virusi
na ugonjwa wa UKIMWI, kifua kikuu pamoja na tiba na kinga ya ugonjwa wa
malaria.
Kwa hivyo Dkt. Shein amemueleza Bw.
Clinton kuwa anaamini jitihada zinazofanywa na Serikali yake pamoja na kuunganisha
nguvu za washirika wa maendeleo mafanikio zaidi yatapatikana.
"Tunaanzisha Taasisi ya Tiba katika
Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ili kufundisha madaktari hapa nchini huku
watumishi wengine wa afya wakipata mafunzo katika Chuo cha Afya hapa
hapa," alifafanua.
Aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo nchi
itakuwa na wataalamu wa afya wa kutosha na watasambazwa maeneo ya vijijini
hivyo suala la uhaba wa watumishi hao litakuwa limepungua kama si kwisha
kabisa.
Dkt. Shein alimhakikishia Bw Clinton kuwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na washirika wa
maendeleo pamoja na mashirika ya kujitolea kama Clinton Foundation katika
kuimarisha utoaji huduma mbalimbali kwa wananchi.
"Napenda nikuhakikishie Serikali
yangu imedhamiria kuwapatia wananchi huduma za afya na nyinginezo na tuko
tayari kuendelea kushirikiana na washirika wetu katika kufikia azma hii,"
alisema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano mzuri
uliopo kati ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Marekani.
"Uh u s i a n o wa Ta n z a n i a na
Marekani ni mzuri sana na umethibitishwa na ziara za mara kwa mara za viongozi
wa nchi zetu," alisema Dkt. Shein na kutolea mfano ziara ya Rais Obama
iliyofanyika nchini Tanzania hivi karibuni.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Marekani,
Bw. Bill Clinton amemwambia Rais wa Zanzibar kuwa amefurahi kuwa taasisi yake
imepata fursa ya kutoa mchango wa kuimarisha utoaji huduma za afya kwa wananchi
wa Zanzibar.
Rais huyo Mstaafu wa Marekani ambaye
amefuatana na binti yake Chalsea yupo nchini ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya
nchi tano barani Afrika kukagua miradi iliyo chini ya ufadhili wa taasisi yake
hiyo. Nchi nyingine ni Malawi, Zambia, Rwanda na Afrika Kusini.
"Zanzibar ni sehemu ya Jumuiya ya
Kimataifa inayounga mkono jitihada na kazi za taasisi yetu hivyo nimefurahi
kufika kwangu hapa leo," alibainisha Bw. Clinton.
Viongozi wengine waliohudhuria mazungumzo hayo ni
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Dkt. Mwinyihaji Makame na Waziri wa Afya Juma Duni
Haji na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Mohamed Saleh Jidawi.
No comments:
Post a Comment