16 August 2013

URANI YAWAPELEKA JELA MIAKA 3 Na Rachel Balama
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, amewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja wafanyabiashara wawili baada ya kukiri kukamatwa na kilo 6.5 za madini ya urani.Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Geni Dudu. Wafanyabiashara hao ni Duncun Mwakanemela (41), mkazi wa Ubungo NHC na Sylivia Anania (42), mkazi wa Manzese ambao wanadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 6,2012 katika maeneo ya Ubungo na Manzese.

Wakili wa Serikali, Charles Anindo, aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa washtakiwa kutokana na madini hayo kuwa na madhara makubwa yanapokuwa mikononi mwa watu ambao hawana leseni wala utaalamu wa kuyatunza.Baada ya ombi hilo, Hakimu Dudu alimuuliza mshtakiwa Mwakanemela kama ana lolote la kuieleza mahakama hiyo ili iweze kumpunguzia adhabu.
Mwakanemela aliiomba mahakama imsamehe akidai anasumbuliwa na shinikizo la damu, anategemewa na mama yake ambaye ni mzee sana na aliyapata madini hayo kwa mshtakiwa mwenzake Anania bila kujua kama ni hatari."Mheshimiwa Hakimu sikujua kama madini haya ni hatari ndiyo maana nilikuwa nakaa nayo ndani... wakati Anania ananipa alisema ni dawa ya mahindi ili nitafute soko ndiyo maana nikayaweka ndani," alisema.
Kwa upande wake, Anania aliiomba mahakama imsamehe kwa kosa alilotenda na kumpunguzia adhabu.Alisema yeye alipelekewa madini hayo hatari na mtu anayeitwa James ambaye walifahamiana miezi sita iliyopita baada ya kumwambia ni dawa ya mahindi."Mheshimiwa Hakimu baada ya kupewa mzigo huo, nilikaa nao ndani na niliuweka pembeni ya kitanda changu kwa sababu sikujua kama ni madini hatari yenye madhara.
Baada ya washtakiwa kutiwa hatiani, Hakimu Dudu alisema adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela imezingatia kifungu cha 11(1) na (2) cha sheria ya nguvu za Atomic (mionzi), namba 7 ya mwaka 2004.
Alisema washtakiwa wamefanya kosa hilo kwa mara ya kwanza hivyo mahakama imezingatia utetezi walioutoa kwani madini hayo yana mionzi ambayo ni hatari kwa viumbe hai.
"Sheria hii inasema mtu akikamatwa lazima alipe faini ya sh. milioni tatu au kifungo cha miaka mitatu jela... nimelazimika kutoa adhabu hii kwa sababu mlikuwa hamjui madhara yake.
"Kwa sababu hatujui mmekaa na madini haya muda gani, Ofisa Jamii awaangalie ndani ya siku 14 mkiwa gerezani na ajiridhishe kama mmeathirika na mionzi ili aifahamishe Serikali muweze kutumikia kifungo cha nje," alisema Hakimu Dudu.
Akitoa ushahidi wake mahakamani hapo, mtaalamu kutoka Tume ya Nguvu za Mionzi, mkoani Arusha, Bw. Leonard Daniel, alisema madini hayo yana madhara makubwa kwa viumbe hai na hayapaswi kuwekwa karibu na watu bila ya kufunikwa kitaalamu.
Alisema madini yaliyokamatwa yanaweza kuleta madhara kwa mtu yeyote aliyeyakaribia katika muda wa miaka mitatu hadi sita kwa kuzaa mtoto mlemavu, kuathirika viungo vya ndani kama ini, figo, mapafu na kubadilisha mfumo wa uzazi

No comments:

Post a Comment