16 August 2013

UKOLONI MAMBOLEO USIVURUGE AMANI YETU



Stella Aron
TANZANIA ni miongoni mwa nchi duniani inayosifiwa kuwa na amani ya kudumu tangu kupata uhuru.
Ni miongoni mwa mataifa yasiyo na historia ya vita duniani na kupata uhuru wake bila kumwaga damu.
Aidha, mataifa ya kigeni yanapenda kuja kuwekeza miradi na makazi huku wanaosikia habari zake wakitamani kufika kuiona amani inayosikika kote ulimwenguni
.
Ni dhahiri kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na hali ya hewa nzuri, mbuga za wanyama, rasilimali za kutosha, maliasili ardhi na madini, misitu, milima na mabonde ambayo pekee yanaifanya kuonekana katika mitazamo tofauti tofauti na hivyo kuwafanya watu wengi kuja kutalii na kufanya makazi au uwekezaji.
Kwa tafakari ya kawaida hapa utagundua amani tunayoisema ni ile ya kutokuwa na vita, mizozo, malumbano, migogoro miongoni mwao.
Aidha, katika nchi yenye vita huwezi kufanya kitu chochote badala yake watu wa taifa husika watakuwa ni wakimbizi na wageni wataogopa kuja kuwekeza katika nchi hiyo.
Mwanzoni mwa miaka ya 1945 baada ya vita vya pili ya dunia, Afrika kuliibuka vuguvugu la kudai uhuru miongoni mwa nchi watawaliwa.
Wakati huo nchi nyingi za Afrika zilikuwa zinatawaliwa na mataifa ya nchi za Magharibi kama Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Ureno na Ugiriki.
Aidha katika kudai uhuru wake nchi hizo zilitumia njia tatu, ambazo moja ni njia ya kudai uhuru kwa kumwaga damu au njia ya mtutu wa bunduki, pili kudai uhuru kwa njia ya kufanya mapinduzi na tatu njia ya amani.
Historia inaonesha kwamba katika kujipatia uhuru wake nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru kwa njia ya vita na umwagaji damu.
Njia hii pekee inazijengea sifa mbaya ya kuwa nchi za vurugu na zisizotaka makubaliano katika kufanya mambo na mipango yake.
Tanzania ilitumia njia ya amani ambayo pekee inaijengea sifa kubwa miongoni mwa mataifa ya Afrika na duniani kwa ujumla.
Na hii itakumbukwa kwamba hata mara baada ya kupata uhuru bado Tanzania iliendelea kuwaheshimu nchi watawala bila kulipiza kisasi kama ilivyokuwa kwa wengine.
Katika historia ya amani iliyopo usipo mkumbuka baba wa taifa, mwalimu Julius Nyerere kwa jitihada zake katika kulipigania taifa kupata uhuru wake pasipo vita pia, kuliongoza taifa kwa amani ya kudumu.
Katika uhai wake Mwalimu alipigania sana suala la amani ambalo kwa kiasi kikubwa linapigiwa kelele na mataifa mengi duniani na mwasisi wa usuluhishi wa migogoro katika nchi za Afrika na mataifa mengine duniani.
Kama utakuwa unashuhudia kinachoendelea katika nchi kama Somalia, Tunisia, Syria, Misri na Libya utakumbuka kilio cha baba wa taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere kuhusu amani barani Afrika.
Katika matazamo huu wa kuingalia Tanzania kama nchi ya amani watu wanatumia vigezo vya utulivu na upendo nchini.
Katika utamaduni wa watu ambao sitausahau ni amani ya Watanzania, tena wale wanaoishi katika maisha ya kawaida na wageni wanaingia kila iitwapo kesho.
Lakini kama tutaendelea kusifia amani hii pasipo kurejea misingi ya haki na usawa miongoni mwa Watanzania itakuwa ni sawa na kazi bure.
Amani ni usalama katika haki na usawa miongoni mwa jamii na hudhihirika katika utekelezaji na utoshelevu wa mipango bila kubughudhi utulivu wa watu wengine.
Katika maana hii utaweza kujiuliza maswali, je mauaji ya albino nchini ndiyo amani tunayojivunia? ukatili dhidi ya watoto yatima na walemavu ndiyo amani tunayoisema? ukatili juu ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali ndiyo misingi ya Tanzania? kutokuhoji mambo na kuonesha hisia ndiyo chanzo cha amani tunayosifiwa na mataifa mengine?
Kutokana na kwamba miongoni mwa Watanzania bado kuna watu wanaendelea kuangamia kutokana na vurugu na matukio yanayoendelea utakuwa ni shahidi kwa tukio lilompata Dkt. Steven Ulimboka baada ya kutekwa na watu wasiojulikana, kwa maelezo yake akiwa katika hali mbaya ya kujeruhiwa na watu hao anadhihirisha jinsi alivyofanyiwa unyama.
Mbali ya kusulubiwa kwa Dkt. Ulimboka pia Mhariri wa gazeti la Mtanzania Absalom Kibanda naye alifanyiwa ukatili na watu wasiofahamika , matukio ambayo hadi sasa yamekuwa historia kutokana na wahusika kufanyiwa ukatili wa kutisha.
Mambo kama haya tumezoea kuyasikia kwenye nchi za kidikteta na kuongozwa kimila ambapo watawala badala ya kutumia njia ya kidemokrasia na kisheria kushughulikia wanaoamini ni maadui zao katika utawala, hutumia genge la wahuni katika taasisi za usalama kuteka raia, kuwatesa, kuwafunga na hata kuwaua.
Sitaki kuamini kwamba Tanzania imefikia huko ukatili huo pekee unaashiria watu wenye mioyo migumu kiasi cha kushindwa kuwa na utu na uvumilivu na kuwepo kwa ukoloni mambo leo.
Pia katika suala la maandamano yanayofanywa nchini na vikundi mbalimbali vya wanaharakati vinaashiria moja kwa moja kukosekana kwa amani ambayo bado tunaendelea kujivunia pasipo kuangalia haki na usawa kama vinatiliwa mkazo.
Tanzania ni jambo la kawaida kufanya utekelezaji wa sera na mipango mpaka pale watu wanapoandamana, kitendo hiki kinachochea hali ya kukosekana kwa amani miongoni mwa wananchi hata kama kuna watu wanatusifia.
Aidha, kitendo cha askari kutumia mabomu kuwatuliza na kuwatawanya watu wakati wa kufanya maandamano kudai haki zao za msingi kinaashiria kukosekana kwa amani miongoni mwa wazawa na inabaki katika historia na nadharia na badala yake hatuwezi kufikia kilele cha amani ya kudumu.
Kama utaratibu huu utaendelea kutumiwa na watawala kama njia pekee ya kutatua matatizo na itakuwa ni njia ya kuwapa kiburi Watanzania kiasi kwamba baadaye nchi inaweza kuingia katika machafuko yasiyovumilika kiasi kwamba jeshi linalotumika kutuliza amani litashindwa kufanyakazi na ndiyo mwanzo wa vita miongoni mwetu.
Kadhalika utakumbuka utofauti uliopo kati ya walionacho na wasionacho (maskini na tajiri). Katika nchi ya Tanzania utabaini kuwa kuna utofauti mkubwa hali inayobainisha moja kwa moja kukosekana kwa usawa miongoni mwa wananchi.
Kitendo hiki kinawanyima amani watu wa hali ya chini kwani hawawezi kuyafurahia maisha yao.
Hata hivyo utofauti unafanywa na viongozi wa ngazi za juu katika serikali unawapa hasira wananchi kutokana na kwamba hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.
Katika mtazamo wa kawaida wapo Watanzania wanaojilimbikizia mali huku wakiendelea kuwakandamiza wengine na ambao kwa bahati mbaya ndiyo wavuja jasho, asilimia kubwa ya wakulima wanafanya kazi usiku na mchana lakini bado hali zao ziko matatani na wakati mwingine wanakosa hata mlo mmoja kwa siku.
Hebu tujiulize amani tunayojivunia ni hii ya kutofautiana kimaendeleo miongoni mwetu kiasi kwamba hatukuzaliwa na kukulia katika nchi moja ambayo kila siku inasemwa maskini.
Je, umaskini tunaousema ni ule wa kukosa kunufaika na maliasili zetu na badala yake kuwanufaisha wachache?
Kama jibu ni ndiyo kwa nini tuendelee kulea mifumo inayowanufaisha wachache na badala yake wengi kukosa amani ya kuwa wazawa katika nchi yao?
Kama utataka kusoma hali ya hewa ya taifa letu kumbuka mara baada ya kukamatwa mwizi wa kuku, jinsi anavyoshughulikiwa, wakati mwingine kumchoma moto.
K a d h a l i k a k ama ama n i tunayojivunia itakuwa ni ile ya utulivu, kukosekana kwa vita, upendo, makubaliano hatuna budi kurudia utamaduni wetu wa usawa na haki miongoni mwetu pasipo ubaguzi wa rangi, hali za kimaisha na kikanda.Kwani umaskini ndiyo utachangia kuvuruga amani iliyopo

No comments:

Post a Comment