26 August 2013

TUZO ZA RAIS KWA WACHANGIA MIRADI YA MAENDELEO YATOLEWANa Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya utafiti madini ya urani yenye mradi wake ujulikanao kama Mto Mkuju ya Mantra ya Tanzania, imeibuka mshindi kwa kunyakua tuzo tatu kwenye Tuzo za Rais katika Tasnia ya Uziduaji kwa makampuni yanayofanya vizuri katika Miradi ya Kijamii na Uwezeshaji (Extractive Industry Corporate Social Responsibility and Empowerment) kwa mwaka 2012.

Kampuni hiyo imeshinda tuzo hizo baada ya kuonekana kuchangia miradi mbalimbali katika sekta ya Elimu, Afya na Ajira na kuibuka mshindi wa pili wa jumla katika kipengele cha Utafiti.
Akizungumzia tuzo hizo za kwanza za Rais katika Tasnia ya Uziduaji ikiangaza Miradi ya Kijamii na Uwezeshaji kwa mwaka 2012, Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania, Asa Mwaipopo, alisema Tuzo hizo ni uthibitisho mkubwa cha mipango mizuri na utekelezaji wa miradi bora ya kijamii waliyonayo.
"Kutambulika huku itakuwa chachu kwa kampuni yetu kuongeza nguvu zaidi katika miradi mbalimbali ya kijamii," alisema
Tuzo hizo zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, ziliandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Jukwaa la Wadau wa Tasnia ya Uziduaji (Extractive Industries Stakeholders Forum - EISF).
Katika tuzo hizo, kampuli zilizoshindanishwa katika tasnia hii ya uziduaji ziligawanywa katika makundi manne. Kulikuwa na kampuni kubwa ya uchimbaji wa madini, kampuni ya kati ya uchimbaji wa madini, kampuni za mafuta na gesi pamoja na kampuni za utafiti wa mafuta, madini na gesi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eliachim Maswi, Kaimu Kamishna wa madini Ally Samaje, Balozi wa Canada nchini Tanzania Alexandre Leveque, na baadhi ya wabunge na wadau mbalimbali kutoka katika tasnia ya uziduaji.

No comments:

Post a Comment