26 August 2013

SERIKALI YATAKIWA KUSIMAMIA UINGIZAJI SARUJI KUTOKA NJE



 Na Grace Ndossa
SERIKALI imeshauriwa kuanzisha juhudi za makusudi zitakazosaidia kukabiliana na uingizwaji wa bidhaa zisizo na viwango zinazoingizwa nchini ikiwemo saruji.Ushauri huo umetolewa na kampuni ya kuzalisha saruji ya Tanzania Portland Cement Company (TPCC).
 Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara iliyotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya TPCC, Pascal Lesoinne, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Saruji Afrika Mashariki (EACPA), alisema suala hilo kama halijapatiwa ufumbuzi litaathiri uhai wa kampuni nyingi nchini na hatimaye kuathiri uchumi kwa ujumla.
"Kampuni nyingi za Tanzania za uzalishaji saruji zinakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa saruji itokayo nje hasa Pakistan," alisema na kuongeza;"Waingizaji wa saruji toka nje wanatumia ipasavyo mianya iliyopo katika mfumo wa forodha na uingiaji wa bidhaa kwa kulipa kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya ushuru wa forodha, hali ambayo inaigharimu nchi hasara ya zaidi ya sh. bilioni 25," alisema, Lesoinne.
Aliongeza kuwa Tanzania haihitaji saruji ya kutoka nje kutokana na uwepo wa kampuni nyingi zinazozalisha saruji hivyo zinaweza fikia mahitaji ya nchi kikamilifu.
Kwa upande mwingine alisema kutopatikana kwa umeme wa uhakika kumeongeza gharama za uendeshaji wa kampuni yake. Alitoa mfano kuwa kampuni yake inatumia zaidi ya dola milioni 2 kwa mwezi ili kuhakikisha umeme mbadala unapatikana pindi umeme wa TANESCO unapokatika.
"Changamoto kubwa inayoathiri uzalishaji wetu ni kutokuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika. Kampuni lazima ihakikishe kuwa wateja wanaendelea kupata bidha zetu kwa wakati wote bila kikwazo," alisema.
Alisema kuwa kampuni ambayo kwa sasa inazalisha zaidi ya tani milioni 1.3 za saruji kwa mwaka itaweza kuzalisha hadi tani milioni 2 kwa mwaka baada ya uzinduzi wa kiwanda chake kipya Oktoba, mwaka ujao.
Kwa upande wake, Mbuge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alieleza wasiwasi kuhusiana na jitihada zinazochukuliwa na mamlaka husika na kuziomba kufanya uchunguzi sahihi kujua ukweli wa suala hilo.
"Hili ni suala nyeti sana. Sisi kama kamati hatuwezi kulifumbia macho kwa kuwa lina athari kwenye maendeleo ya uchumi wa nchi yetu," alisema Kafulila.
Mkurugenzi wa Viwanda katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Eliness Sikazwe, alisema Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, tayari ameteua kamati ya wanachama saba kuchunguza suala hilo na kuongeza kuwa kamati hiyo itatoa ripoti baada ya uchunguzi kukamilika.

No comments:

Post a Comment