Na LIlian Justice, Morogoro
BARAZA la Madiwani wa
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro limetenga kiasi cha sh. milioni 40 kwa ajili
ya kufanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji walioingia kinyume cha sheria
wilayani humo. Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema kutengwa kwa fedha hizo za
kuendesha operesheni ya kuwaondoa wafugaji na kuhakiki mifugo iliyopo wilayani
humo kutasaidia kudhibiti tatizo la ongezeko kubwa la mifugo inayoingia visivyo
halali.
Alisema ni vyema operesheni hiyo ikafanyika wakati wa kiangazi
kabla ya shughuli za kilimo kuanza kwani ongezeko la mifugo husababisha
migogoro inayopelekea ugomvi na hatimaye wananchi kupoteza maisha. Aliwasisitizia madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali
kushirikiana katika zoezi hilo ili kufanyika operesheni hiyo wakati itakapoanza
na kuacha kutetea watu watakaobainika wameingia bila utaratibu kwani wenye
mamlaka ya kusema ni wananchi wenyewe wa vijiji husika na si wao.
Pia aliwaagiza watendaji katika halmashauri hiyo kuanzia ngazi ya
vijiji kushirikiana katika kufanikisha zoezi la ujenzi wa madarasa ili
wanafunzi watakapochaguliwa kusiwe na tatizo la uhaba wa madarasa. "Pamoja na kusimamia suala la ujenzi wa madarasa lakini pia
msimamie suala la uboreshaji wa elimu ya msingi na sekondari kwani kumekuwa na
tatizo la baadhi ya wanafunzi kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari lakini
hawajui kusoma na kuandika," alisema.
"Suala la uboreshaji wa elimu ya sekondari liende sambamba na
uboreshaji wa elimu ya msingi kwani kwenye shule ya msingi hakuna madarasa,
nyumba za walimu matundu ya vyoo kwa wanafunzi," aliongeza kusema. Naye Diwani wa Kata ya Lundi, Ally Mkata alisema katika shule ya
sekondari Lundi kuna matumizi mabaya ya fedha kwa mwalimu mkuu huyo kutokana na
shilingi milioni kumi na tatu kutumika kinyume na taratibu.
Akijibu tuhuma hizo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Charles Madiga
alisema kuwa, suala hilo linafanyiwa kazi na kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo
ataanza kukatwa fedha hizo kwenye mashahara wake wa mwezi Agosti. Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kingo aliagiza pamoja na mkuu
wa shule hiyo kukatwa mshahara wake lakini ni vyema pia akaelezwa kuwa
alichokifanya ni kosa kinyume na utumishi wa umma na kwamba hatua nyingine
zichukuliwe dhidi yake.
Naye Diwani wa Kata ya Kiroka, Robert Serasera alisisitizia
watumishi wa halmashauri kusaidia suala la upimaji wa maeneo kwa wananchi
kwenye vijiji vya halmashauri hiyo ili kuepusha usumbufu unaotokea kutokana na
maeneo yao kutopimwa kisheria
No comments:
Post a Comment