26 August 2013

TAHLISO YAWAVAA WANAFUNZI WANAOTUMIKA KISIASA NCHININa Darlin Said
TAASISI ya Wanafunzi wa Vyuo Vya Elimu ya Juu (TAHLISO) imelaani vikali matukio yaliyojitokeza katika mkutano wa baadhi ya viongozi wa Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vya elimu ya juu hapa nchini uliofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni na kudai kuwa ni ulikuwa kinyume na maadili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Mtendaji wa TAHLISO, Donati Salla alisema mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga, Maradhi na Umaskini (FPID) na sio TAHLISO kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Alisema katika mkutano huo mbali na mambo yaliyozungumzwa kubwa lililokuchukua uzito mkubwa ni suala la ni nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Mwaka 2015.
Kutokana na hali hiyo Salla alisema TAHLISO inasikitishwa na tukio hilo kwani Serikali yao inashughulika na masuala ya wanafunzi na ubora wa taaluma itolewayo katika chuo husika na masuala mengine ya kitaifa lakini si ushabiki wa kisiasa au kutetea kundi au maslahi ya watu fulani.
"Jukumu la vyama vya siasa vilivyosajiliwa na kutambulika kiserikali kukaa na kuchagua au kuteua wajumbe wanaogombea nafasi mbalimbali za kisiasa iwe katika chama, serikali au vinginevyo lakini hilo siyo jukumu la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu,"alisema Salla.
Mbali na hilo alisema vikao vyote vinavyohusu mjumuiko wa Serikali za wanafunzi vinapaswa kuitishwa na kuratibiwa na TAHLISO na siyo taasisi nyingine yoyote.
Hivyo TAHLISO inatoa onyo kali kwa viongozi wa Serikali za Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambao walishiriki kwenye mkutano huo na kuwataka kutorudia tena na kuwataka kutimiza jukumu lao la kusoma na kujifunza taaluma zao kwa taratibu zilizoainishwa na chuo husika.

No comments:

Post a Comment