29 August 2013

POLISI KUSHIRIKIANA NA WATAALAMU WA MAJENGO Na Gladness Mboma
JESHI la Polisi nchini limesema liko tayari muda wowote kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Ujenzi (AQRB) ili kuhakikisha ujenzi wa majengo yote nchini unashirikisha wabunifu majengo.

Sambamba na wakadiriaji ujenzi waliosajiliwa, wenye sifa stahili ili kulinda usalama na mali za watumiaji. Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo nchini, Paul Chagonja kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema wakati alipokuwa akimwakilisha katika mkutano wa pamoja kati ya jeshi hilo na bodi hiyo.
Alisema kuwa, wanatambua majukumu ya AQRB kisheria hasa kuwajibisha wataalamu na waendelezaji wa ujenzi wanaokiuka sheria na hata sheria nyingine za nchi. "Ombi langu ni kuwa wale wanaokiuka sheria wawajibishwe na bodi kwa mujibu wa sheria yenu na wale ambao wanatakiwa wapelekwe mahakamani tushirikiane ili sheria ichukue mkondo wake," alisema.
Alisema kuwa, Jeshi la Polisi linashukuru kutambua dhamira ya kuendeleza ujenzi wa makazi ya askari wao na kwamba wamekuwa wakiwatumia wabunifu majengo, wakadiriaji ujenzi, wahandisi na makandarasi waliosajiliwa na taasisi husika na wataendelea kuwatumia.
Chagonja alisema, kwa kufanya hivyo hata jamii haitaona jambo la ajabu pale watakapokuwa wanachukua hatua za kisheria kwa wale ambao wanajenga makazi yao bila ya kuwatumia wataalamu.
Alisema kuwa, wataendelea kuwatumia kikamilifu wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ambao ni watumishi katika jeshi lake na kuwaendeleza wale ambao hawajasajiliwa na bodi ili hatimaye wawe na sifa zinazotakiwa.
"Jambo muhimu tunaomba mtupatie ushirikiano wa karibu, hasa pale ushahidi unatakiwa kutoka kwenu upatikane kwa muda mwafaka, ikumbukwe kila fani ina wataalamu wake, hivyo ushirikiano wenu katika kutoa taarifa za kitaalamu utasaidia sana wataalamu wa jeshi letu kuchukua hatua kwa wakati na wepesi," alisema.
Chagonja alikiri kuwa, uelewa wa jamii kuhusu bodi na majukumu ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ni mdogo sana na kwamba hata wao kama sehemu ya jamii kuna baadhi yao hawafahamu majukumu ya bodi na yale ya wataalamu.
"Hivyo dhamira yenu ya kujitangaza ni nzuri, kwani ndio njia pekee ya kuwafanya wananchi watii sheria bila shuruti na kupunguza kesi zinazotokana na watu kutenda mambo kwa mazoea bila kufuata sheria,"alisema.
Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Ambwene Mwakyusa alisema lengo la mkutano huo ni kujitambulisha kwa wadau wa kusimamia sheria kwa makosa ya jinai ili kupanua uelewa wa majukumu ya bodi na pia umuhimu wa wataalamu wanaowaratibu katika sekta ya ujenzi nchini.
Alisema, bodi ina jukumu la kuingia na kukagua miradi ya ujenzi kwa lengo la kuhakikisha imebuniwa na kusimamiwa na wataalamu waliosajiliwa na bodi, miradi ambayo imesambaa nchi nzima kufikia Juni 30, mwaka huu ambapo bodi ilikuwa imesajili wataalamu 834 na kampuni 276.
 

No comments:

Post a Comment