Na Respice Swetu, Kasulu
ZAIDI ya sh. bilioni nne zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa
Chuo cha Ufundi Nyamidaho kinachojengwa katika Tarafa ya Makere wilayani Kasulu
Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza
juzi ofisini kwake, Ofisa Elimu Ufundi wilayani Kasulu, Gerard Nkona alisema,
chuo hicho kinajengwa kutokana na msaada wa Shirika la Kimataifa la World
Vision linalofanya shughuli zake wilayani humo.
Shirika
hilo linalojishughulisha na utoaji wa huduma za kijamii kupitia miradi
mbalimbali ya kimaendeleo nchini, tayari limetoa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kwa
ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa chuo hicho.
"Ambapo
zaidi ya shilingi milioni tano, kati ya hizo zimetumika hadi sasa kwa kazi
inayoendelea ya ujenzi wa jengo la utawala, madarasa na mabweni," alisema Ofisa
huyo.
Pia
alisema, chuo hicho baada ya kukamilika kitatumika kutoa mafunzo katika fani za
ufundi umeme, seremala, uashi na sayansi kimu na baada ya hapo zitaongezwa fani
zingine kadri ya maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho ambacho kinatarajiwa kuwa kikubwa
kuliko vyuo vya ufundi vilivyopo katika ukanda wa Magharibi mwa Tanzania.
Alifafanua
pia kuwa, ujenzi wa chuo hicho ulioanza mwaka 2012 umepangwa kutekelezwa kwa
awamu tatu huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, mwaka 2014 lengo
likiwa ni kupokea wanafunzi wa kujiunga na chuo hicho katika kipindi cha muhula
wa masomo kitakachoanza mwezi Julai mwakani.
"Tunawashukuru
wakazi wa Kijiji cha Nyamidaho kwa kukubali kutoa ardhi yenye ukubwa wa hekari
40 ili kupisha ujenzi wa chuo hicho na halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa
kuchangia gharama za michoro," alisisitiza Nkona huku akitoa wito kwa
vijana kuichangamkia fursa hiyo.
Hata
hivyo, kujengwa kwa chuo hicho kunatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Wilaya
ya Kasulu na maeneo jirani.
No comments:
Post a Comment