Na Thomas
Mtinge, Dodoma
MAKATIBU wa Jumuiya
ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ngazi ya mikoa na wilaya nchini
wameagizwa fedha zilizowekwa kwenye benki ya CRDB kwa ajili ya kuanzisha Family
Benki, zirudishwe mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
Agizo
hilo lilitolewa mjini Dodoma juzi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ya
CCM, Abdallah Bulembo, ambapo alisisitiza kuwa hatua hiyo inatokana na kile alichodai
kutoridhishwa kwake na mwenendo mzima wa kukusanya na kutunza fedha za
kuanzisha benki hiyo kwa kuingia ubia na kampuni binafsi (jina tunalo).
Taarifa
inaonesha kuwa akaunti hiyo ina sh. milioni 5 wakati fedha zinazodaiwa
kukusanywa na makatibu hao ni zaidi ya s. milioni 20.
Bulembo
alitoa agizo wakati akizungumza na Wajumbe wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo katika
kikao chake kilichofanyika Dodoma.
“Ndugu viongozi wenzangu mimi mpaka sasa sijaridhishwa kabisa na hatua
zilizopo sasa za uanzishwaji wa benki hii. Binafsi napata shaka kubwa tusije tukanzisha DECI
badala ya benki; maana hata fedha zilizotolewa na makatibu wetu
kama ziko kwenye
mikono salama," alisema na kuongeza;“Jamani, nazidi kupata shaka na
kutokuwa na imani na wenzetu hawa wanaoshughulika na uanzishwaji wa benki hii
kwa sababu hata ile hundi ya sh. milioni 10 iliyotolewa mbele ya Mwenyekiti
wetu, (Rais Jakaya Kikwete) wakati akizindua benki hii pale Ukumbi wa Chuo cha
Mipango, fedha zake mpaka sasa hazijulikani zilipo, sasa kwanini nisiwe na
shaka?,” alihoji Bulembo.
Bulembo alisema tayari ameshawaandikia
barua makatibu hao akiwataka kusitisha kupeleka fedha benki kwa ajili ya benki
hiyo mpaka hapo atakapopata ufafanuzi zaidi wa zilipo fedha zilizotolewa awali
na kujiridhisha na jitihada za kuendelea na mpango huo.“Kama kuna watu waliokula fedha hizi
wazirudishe haraka vinginevyo watashtakiwa bila kujali nyadhifa zao,” alisema.
Wakichangia kwa nyakati tofauti kuhusu
kuanzishwa kwa benki hiyo, Wajumbe wa Baraza Kuu hilo wameeleza kusikitishwa
kwao na siri nzito inayofanywa na viongozi wa jumuiya hiyo taifa kuhusu kiasi
cha fedha zilizokusanywa hadi sasa.Mjumbe wa Baraza hilo, William
Malecela, aliwataka wajumbe wenzake wasikubali kupoteza muda kwa ajili ya
kujadili kuanzishwa kwa benki hiyo.
“Tuna mambo mengi ya kujadili hapa tena
ya msingi, hivyo tusikubali kujadili benki ambayo ni kiinimacho. Hakuna benki
hapa bali tunapoteza muda wetu bure.“Hawa waliyoleta wazo la kuanzisha
benki hii hawafai na kwa sheria za nchi kama vile ya China, hawa wangehukumiwa
kunyongwa au kupigwa risasi kwa sababu wametudanganya kwani walikuja katika
jumuiya hii au kwa vile waliikuta ikiwa imekufa,” alisema Malecela.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa jumuiya
hiyo mkoani Mbeya, Fatuma Kasenga, alishauri hatua za haraka zichukuliwe ili
kujua ukweli wa kuanzishwa kwa benki hiyo.Alisema ni jambo la kutia aibu kuona
benki iliyozinduliwa na Mwenyekiti wa CCM, kwa ajili kuinua uchumi wa jumuia
yake kuwa ya kisanii zaidi.
“Tusikubali kukidhalilisha Chama chetu
wala rais wetu. Leo ndiyo nimejua kwamba siasa ni uongo. Viongozi wetu wa
jumuiya wanajigamba kwamba kuna benki kumbe si lolote wala si chohote,”
alisema.
Benki hiyo iliyozinduliwa na Rais Kikwete iliingiwa ubia baina ya
Kampuni mmoja (jina tunalo) na Jumuiya ya Wazazi.
No comments:
Post a Comment