23 August 2013

POLISI 'FEKI' WAPO - NCHIMBI



Na Grace Ndossa
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amekiri ndani ya Jeshi la Polisi kuna askari ‘feki’ aliowapa jina la “Makanjanja”, kama ilivyo katika sekta nyingine ingawa Serikali haipendezwi na hali hiyo.Dkt. Nchimbi aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tume iliyoundwa na jeshi hilo kuchunguza matukio yaliyolalamikiwa dhidi ya askari polisi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro pamoja na Kigoma.

Alisema kutokana na hali hiyo, wataanza kufuatilia kwa kina askari waliostaafu au kufariki ili kujiridhisha kama walirudisha sare walizokuwa wakizitumia wakiwa kazini.Aliongeza kuwa, vitambaa vya sare za polisi vinapatikana katika maduka mbalimbali hivyo mtu yeyote anaweza kununua, kushona na kuweka nembo za polisi hivyo ni vigumu kudhibiti hali hiyo.“Ndani ya Jeshi la Polisi kuna askari makanjanja (Feki), kama ilivyo kwa sekta nyingine, hakuna mtu anayependa wawepo, hivi sasa askari ambao watapatikana na makosa ya uhalifu, viongozi wanaohusika kuwasimamia watashushwa vyeo na wahusika watafukuzwa kazi,” alisema Dkt. Nchimbi.
Alisema ameipitia ripoti ya tume ambayo imewasilishwa kwake na kufuata ushauri uliotolewa wa kuwachukuliwa hatua askari waliohusika na matukio mbalimbali kwa kuwafukuza kazi na wengine kuvuliwa madaraka.Dkt. Nchimbi alisema askari saba wamefukuzwa kazi kwa sababu ya kujihusisha na matukio ya uhalifu ambao wengine walikamatwa na bangi mkoani Kilimanjaro, fuvu la kichwa cha Binadamu (Morogoro) na kusababisha mauaji ya wafanyabiashara Mjini Kasulu, mkoani Kigoma.
“Tukio la askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mkoani Arusha Ex F.1734 CPL Edward na G. 2434PC George wa Kituo cha Polisi Ngarananyuki, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, walifukuzwa kazi baada ya kukiri kosa la kusafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi,” alisema.Aliongeza kuwa, gari la polisi PT 2025, aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likisafirisha bangi yenye uzito wa kilogramu 540, yenye thamani ya sh. milioni 81 ambalo lilikamatwa mkoani Kilimanjaro, Mkuu wa Kikosi Mrakibu wa Polisi Ramadhani Giro, amevuliwa madaraka aliyokuwa nayo.
“Mrakibu Giro alishindwa kusimamia maofisa walio chini yake, askari mwingine Inspekta Isaack Manoni, amesimamishwa kazi na kuagiza ashtakiwe kijeshi akidaiwa kumtorosha mtuhumiwa hatari Ex F.1734 CPL Edward, aliyekuwa dereva wa gari la polisi ambalo lilikamatwa na bangi, Kilimanjaro,” alisema.Alisema askari wengine wawili, Inspekta Salimu Juma Kingu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na Inspekta Mikidadi Galilima, wote wamepewa onyo kali katika utendaji kazi.
Dkt. Nchimbi aliongeza kuwa, askari mwingine ASP Francis Duma PF.15828, aliyekuwa kiongozi wa kukamata gari ambalo lilibeba bangi, amepandishwa cheo kuwa Mrakibu wa Polisi.Alisema Inspekta Jamal Ramadhani na Inspekta Juma Mpamba ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Upelelezi, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, wamevuliwa madaraka kwa kuonesha udhaifu katika utendaji kazi kwa kutowasimamia kikamilifu askari walio chini yao baada ya kukamatwa na fuvu la kichwa cha binadamu.
Hata hivyo, Dkt. Nchimbi alisema Mkuu wa Kituo cha Upelelezi Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, ASP Bendarugaho, amevuliwa madaraka kwa kutokuwa makini kwenye kusimamia upelelezi wa jalada la kesi ya mauaji ya marehemu Gasper Sigwavumba ambapo upelelezi wa kesi hiyo utaanza upya ili haki itendeke

1 comment:

  1. sasa kama walinda usalama wako hivi, nadhani iko haja ya kufanya utafiti wa kina ili kubaini ni kitu gani kinawafanya walinzi hawa wa amani hasa siku hizi wanafanya vitendo hivi. Ni je wanatumwa na wakubwa wao au wanajituma wao wenyewe. Bila ya kufanya utafiti wa kina na kujua chanzo cha kufanya hivyo wananchi watakosa kabisa imani na vyombo hivyo ambapo vituklo kama hivyo vikizidi kuendelea kila kukicha.

    ReplyDelete