23 August 2013

ASKARI 'FEKI' AFIKISHWA KORTINI' AKANA MASHITAKA



MKAZI wa Kimara, Dar es Salaam, Bw. James Hussein Hassan (45), jana amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashtaka mawili, anaripoti Rachel Balama.Mashtaka hayo ni kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na kukamatwa na sare za Jeshi la Polisi.

Ilidaiwa na wakili wa Serikali, Bw. Nasor Katuga mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joyce Minde kuwa, Agosti 14 mwaka huu, eneo la Kinyerezi Mnara wa Voda, mshtakiwa alifanya udanganyifu wa kujitambulisha kwa Inspekta Gabriel Chiguma kuwa yeye ni askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
Katika shitaka la pili, inadaiwa Agosti 14 mwaka huu, eneo la Kinyerezi Mnara wa Voda, mshtakiwa alikamatwa na sare za polisi ambazo ni kofia, mkanda, jaketi pamoja na nembo ambavyo vyote ni mali ya jeshi hilo.
Mshtakiwa alikana mashtaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini. Alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye makazi ya kudumu ambao watasaini hundi ya sh. milioni saba kila mmoja. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 5 mwaka huu

No comments:

Post a Comment