27 August 2013

OMAN WAVUTIWA KUWEKEZA ATCL



Na Salim Nyomolelo
SHIRIKA la Maendeleo na Uwekezaji la Alhayat kutoka nchini Oman litatumia dola za Kimarekani milioni 100 kuwekeza katika Shirika la Ndege nchini (ATCL), sambamba na kujenga jengo la ghorofa 25 katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam kama serikali ikiridhia kusaini mkataba nao.

Shirika hilo lilifanya ziara Dar es Salaam jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) ili kujionea fursa zilizopo pamoja na changamoto kwa lengo la kuwekeza.  
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara hiyo, Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Shekhe Salim Bin Abdullah alisema kuwa wamepania kuwekeza ATCL ambapo wataingiza ndege nane za kisasa mara baada ya kukubaliana na serikali ikishapitia rasimu ya mkataba.
Shekhe Abdullah alisema kuwa, licha ya kuwekeza ATCL, pia litaboresha miundombinu pamoja na kuweka vifaa vya kisasa katika uwanja huo ili kuboresha usalama kwa wateja.
Alisema kuwa, shirika limepania pia kujenga jengo kubwa la kisasa katika eneo la Posta ambalo litakuwa na ghorofa 25 na kuongeza kuwa huduma mbalimbali zitakuwepo ikiwa ni pamoja na Supermarket ambayo itakuwa kubwa hapa nchini, maduka mbalimbali, hoteli, huduma za simu, maeneo ya maegesho ya magari pamoja na ofisi za shirika la ndege.
"Ili kwenda sawa na mfumo huo, tutachukua baadhi ya wafanyakazi kuwapeleka Oman kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimbali ya kisasa, hasa katika utoaji wa huduma wa viwanja vya ndege ambao nao watatoa mafunzo kwa wenzao," alisema Shekhe Abdullah.
Alisema kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kujenga mazingira kwa ajili ya kuwapata na kuwavutia wateja ili kupanua wigo wa kutoa huduma bora na si kufanya kazi kiholela jambo ambalo litasababisha wateja kukimbia.
Hata hivyo, miongoni mwa mapendekezo aliyotoa Shekhe Abdullah ni pamoja na kuongeza kamera za kisasa zenye uwezo mkubwa, kuboresha kitengo cha zimamoto na uokoaji, kuboresha hali ya usalama ili kuepukana na upotevu wa mizigo ambao unaweza kujitokeza pamoja na vifaa vya kisasa vya kukagulia mizigo ambapo wakishaingia mkataba na serikali atasaidia kuviweka.
Alisema kuwa, ziara aliyoifanya Rais Jakaya Kikwete nchini Oman hivi karibuni iliwavutia kuja kuwekeza baada ya kukaribishwa wafanyabiashara ambapo aliongeza kuwa Tanzania na Oman zina historia nzuri pamoja na kuunda undugu kutokana na kuoana.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harisson Mwakyembe alisema kuwa, Serikali itapitia rasimu ya mkataba huo kwa kina kabla haijaingia makubaliano ya shirika hilo licha ya wao kuwa na nia nzuri ya kuwekeza.

1 comment:

  1. .."Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harisson Mwakyembe alisema kuwa, Serikali itapitia rasimu ya mkataba huo kwa kina kabla haijaingia makubaliano ya shirika hilo licha ya wao kuwa na nia nzuri ya kuwekeza.".. Hapo Mwakyembe umesema maana Oman si kama wameendelea katika huduma na biashara za ndege,Oman air haina sifa nzuri kiusalama duniani,sasa leo wachukuwe watu wakajifunze kwao kwanini?nsi heli tupeleke watu Ethiopia au Qatar?Katika enzi hizi za utandawazi watanzania tusiwe wavivu wa kufanya research za haraka haraka kwenye mtandao,tusitegemee elimu darasa tu,huu ni wakati tofauti.Nimejaribu kupata jina la kampuni na la mkubwa wao alietajwa humu kwenye mtandao nikaambulia patupu.Hapa ina maana mwandishi hakuhakiki kupata majina sahihi au ndio mambo ya richmond ya kampuni za briefcase.

    ReplyDelete