13 August 2013

MTOTO ALIYEUNGANA MIDOMO AZALIWA LINDI



 Na Said Hauni, Lindi
MKAZI wa Kata ya Nyengedi, Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, amejifungua mtoto huku midomo yake ikiwa imeungana hali inayomfanya kupata shida wakati wa kunyonya maziwa ya mama yake.Habari kutoka eneo hili zilizothibitishwa na wazazi wa kijana huyo, zinaeleza mtoto huyo amezaliwa katika Zahanati ya kijiji hicho, Agosti 2 mwaka huu usiku
. Waandishi wa habari waliofika eneo hilo walifanikiwa kumshuhudia mtoto huyo wa kike midomo yake miwili ya juu na chini ikiwa imeungana ikiwemo na pua huku matundu mawili sehemu ya mdomo wake.
Baadhi ya wananchi pamoja na Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Thomas Ngomo wamesema mtoto huyo wa kike amezaliwa katika zahanati hiyo.
Aidha walisema hili ni tukio la kwanza kutokea kwa mwanamke kuzaa mtoto akiwa na matatizo ya aina hiyo katika kijiji chao tangu kianzishwe miaka 1965.
Mama wa mtoto huyo ameliambia gazeti hili kwamba ni kama mkosi kwake ikizingatiwa ni kijana wake wa kwanza mwenye ulemavu kati ya watoto wawili aliokuwa nao.
"Huyu ni mtoto wangu wa pili, lakini huyu wa kwanza sio kwa mume niliyenaye sasa, Mwenyezi Mungu ameamua kunijalia, hivyo siwezi kumfanyia ubaya wowote kama wafanyavyo baadhi ya wanawake wenzangu, ninamlea kama kawaida kwani yote yametokana na mapenzi yake mungu," alisema Hadija.
Alisema kwa sasa mtoto wake huyo anatumia kumnywesha maziwa yake kwa njia nyingine ikiwemo ya kuyakamua kisha kumuwekea kwenye chombo na kummiminia kupitia kwenye matundu mawili yaliyopo eneo ambalo mdomo umeungana.
Mume wa mwanamke huyo alisema baada ya kuzaliwa kwa kijana wake walimpeleka Hospitali ya Nyangao,iliyopo ndani ya Halmashauri hiyo,ili kutafuta ufumbuzi wake,lakini wataalamu wamemshauri kumpeleka Jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Kairuki kwa utaalamu zaidi.
"Hivi sasa nipo katika kujitafutia nauli niweze kumsafirisha kijana wake akapate tiba itakayomuwezesha kijana wangu aweze kunyonya vizuri kuliko ilivyo sasa," alisema Salum Saidi.

No comments:

Post a Comment