19 August 2013

MILIONI 10/- ZACHANGWA KUUNGANISHA CHF



Na Mwandishi Wetu, Njombe
MAMLAKA ya Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na Program ya Tunajali zimechangisha zaidi ya sh.milioni 10 kuwawezesha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu mkoani humu kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

CHF hufanya kazi kiwilaya kugharamia huduma za afya kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kwenye maeneo ya vijijini. Katika mpango huo mwananchi anatakiwa kulipa kiwango fulani cha fedha wakati wa usajili kisha pamoja na kaya yake hupata huduma bora za afya kwa mwaka mzima.
Uchangiaji watoto hao ulikuwa ni sehemu ya uzinduzi wa kampeni iitwayo “Jali Afya Yako, Jiunge na CHF Leo” inayofanywa na Program ya VVU na UKIMWI ya Tunajali inayofadhiliwa kwa msaada wa Watu wa Marekani kupitia Shirika la Misaada ya Kimataifa (USAID) kama sehemu ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).
Katika shughuli hiyo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Aseri Msangi, ambapo kati ya fedha hizo ahadi ilikuwa ni sh. 8,037,000 na fedha taslimu zilikuwa sh. 2,138,000.
Fedha zilizopatikana katika hafla hiyo zinatosha kuwaunganisha watoto 5,087 na CHF kwani kundi la watoto watano linagharimu sh. 10,000 kujiunga na Mfuko huo.
Akizindua kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha watu kujiunga na CHF, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, alisema watu wengi bado hawajajiunga na mfuko huo na matokeo yake ni hukosa huduma za afya wanapozihitaji kwani hushindwa kulipa sh. 2,000 ya papo kwa papo ya usajili wanayotakiwa kulipa watu wasio na bima ya afya kila wanapoumwa.
Mkurugenzi Uendeshaji wa Tunajali, Dkt. Joseph Ng’weshemi, alisema kuwa changamoto za upatikanaji wa huduma za afya za kutosha na endelevu bado ni kubwa nchini na hilo ndilo lililoisukuma Programu yake kubuni.
Dkt. Ng’weshemi alisema kuwa umaskini na kutokuwa na kipato cha uhakika vimewafanya wananchi wa kawaida kuwa na wakati mgumu kuchangia mahitaji yao binafsi ya huduma za afya.
Serikali nayo kwa upande wake imekuwa ikijaribu kugawa rasilimali zake kwenye vipaumbele vyake kikiwemo cha afya ambapo inategemea sana wahisani.
Kampeni hiyo itakayofanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Njombe, itaielimisha jamii kuhusu dhana ya bima ya huduma za afya na wajibu wa wananchi katika kuwekeza katika afya zao.
Pia itahamasisha wanajamii na hasa wale wanaoishi na VVU kujiunga na CHF hasa ikizingatiwa kuwa maambukizi ya VVU mkoani hapa ni makubwa zaidi nchini ambapo ni asilimia 14.8.

No comments:

Post a Comment