MAHAKAMA ya Rufaa Dar es Salaam
imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Kasulu Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Nsanzugwako,
aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora uliotolewa Mei
3,2012, anaripoti Rehema Mohamed.
Nsanzugwako
alifungua kesi ya uchaguzi katika Mahakama Kuu ya Tabora kupinga matokeo ya
ubunge wa Jimbo hilo mwaka 2010 yaliyompa ushindi, Agripina Buyogera, kupitia
Chama Cha NCCR Mageuzi baada ya kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo.
Katika kesi
hiyo Mahakama Kuu Kanda ya Tabora ilimpa ushindi Bugogera.
Uamuzi wa
kutupa rufaa hiyo ulitolewa katika Mahakama ya Rufaa jana na jopo la majaji
watatu waliokuwa wakiisikiliza ambao ni Jaji Nathali Kimaro, akisaidiana na Jaji
Salum Massati na Jaji William Mandia.
Katika uamuzi
huo wa kutupa rufaa hiyo, majaji hao walisema kuwa baada ya kuangalia mwenendo
mzima wa shauri hilo wameona kuwa Jaji Haruna Songoro wa Mahakama Kuu ya Tabora
alitimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuchambua ushahidi uliowasilishwa
mahakamani hapo wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa na hawakubaliani na
maelezo ya Nsanzugwako kuwa mahakama hiyo haikuchambua ushahidi huo kama
ilivyotakiwa.
Walisema kuwa,
katika hoja ya kwamba Nsanzugwako alitolewa maneno ya kashfa katika mikutano ya
kampeni ya Bugogera walisema kuwa, Jaji Songoro alikuwa sahihi kutilia mashaka
kama mlalamikiwa alikashifu.
Ilielezwa kuwa,
kwa mujibu wa sheria ya maadili ya uchaguzi ambayo vyama vyote vilisaini
inapotokea mgombea ametolewa lugha ya kashfa au matusi anatakiwa kwenda Tume ya
Uchaguzi kutoa malalamiko ambapo kwa upande wa Nsanzugwako hakufanya na hivyo
kufanya malalamiko yake kutokuwa na nguvu.
Kutokana na
sababu hizo,majaji hao wametupilia mbali rufaa hiyo kwa gharama.
Katika rufaa
yake Nsanzugwako malalamiko makubwa ni kwamba Buyogera wakati wa mikutano yake
ya kampeni, alimtolea maneno ya kashfa akimtuhumu mchawi na alishiriki kumuua
aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Tadi Magayane.
Pia alidai kuwa, Buyogera alimtuhumu kuwa
ni mkorofi, alikuwa anashiriki uchaguzi kupitia ‘chama cha wala rushwa na mwizi
kwa sababu alifuja fedha za jimbo hilo sh. milioni 31.”
No comments:
Post a Comment