16 August 2013

MADIWANI WAMWEKEA NGUMU MWEKEZAJINa Derick Milton, Simiyu
MA D I W A N I w a Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi wameazimia kusimamisha shughuli za kampuni ya uwekezaji ya Red Hill Nickel iliyoingia mkataba na Serikali kuchimba madini aina ya Nickel katika Kata ya Dutwa wilayani humo, kwa kile kinachodaiwa kuwa kampuni hiyo kuanza shughuli za utafiti wa madini hayo bila ya halmashauri kuhusishwa.

Kampuni hiyo iliyoingia mkataba na Wizara ya Nishati na Madini kuchimba madini hayo ilianza shughuli za utafiti wa maeneo yanayomilikiwa na wananchi kwa kuchimba mchanga na kuacha mashimo, bila ya kulipia ushuru ndani ya halmashauri husika.
Hatua hiyo ya azimio la kusitisha shughuli zote zinazoendeshwa na kampuni hiyo ilifikiwa katika kikao cha Baraza la madiwani hao kilichofanyikia katika mjini humo ili kuweza kupata ufafanuzi juu ya halmashauri itakavyonufaika na uchimbaji wa madini hayo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti madiwani hao walieleza kuwa mwekezaji huyo amekuwa akialikwa katika vikao mbalimbali vya halmashauri ili kukutana na madiwani, kwa ajili ya kuweza kutoa ufafanuzi juu ya halmashauri itakavyonufaika.
Waliongeza kuwa mbali na kuombwa kila kikao cha baraza kwa mwekezaji huyo kuhudhuria ili kuweza kutoa fafanuzi juu ya suala hilo, kampuni hiyo imekuwa ikitoa sababu mbalimbali kwa kuandika barua ya kujulisha kwao kutoshiriki vikao hivyo kwa sababu mbalimbali.
Akitoa ushauri kwa madiwani hao Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Engelberth Kalekona aliwataka wadiwani hao kuandika barua kwa Waziri mwenye dhamana ya madini yenye madai hayo ili kuweza kumsimamisha mwekezaji huyo.
Alisema Halmashauri haina uwezo wa kuweza kusimamisha shughuli zinazoendelea kufanywa na mwekezaji huyo, kwa kuwa mkataba wa uchimbaji wa madini hayo uliingiwa baina ya Wizara husika na mwekezaji na siyo halmashauri na mwekezaji huyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mabula Magamula aliagiza kuandikwa barua ya kwenda moja kwa moja katika Wizara ya Nishati na Madini ili kumuomba Waziri kusitisha kazi hizo hadi kampuni hiyo itakapotoa ufafanuzi wa kina juu ya kunufaika kwa halmashauri na uchimbaji huo.

No comments:

Post a Comment