Na Shaban Mbegu
KOCHA mkuu wa timu ya Simba Abdallah
Kibaden amesema kuwa hana hofu na kikosi chake, japokuwa amekiri kuwa kitakuwa
na changamoto nyingi.Simba msimu huu
ilitema baadhi ya wachezaji wengi waliokuwa katika timu hiyo msimu uliopita
kutokana na sababu mbalimbali na kutengeneza kikosi kipya huku wakiwapa zaidi
nafasi vijana.
Baadhi ya
wachezaji waliotemwa ni Haruna Moshi, Juma Nyoso, Juma Kaseja, Amiri Maftah,
Abdallah Juma, Mussa Mude, Salum Kinje Komabil Keitha, Paul Ngelema na Felix
Sunzu.Kibadeni
aliyezaliwa Oktoba 11, 1949, Mbagala Kiburugwa, Dar es Salaam alisema anaamini
kikosi chake kitaanza vizuri ligi hiyo japokuwa kimeundwa kipya.
Kibadeni ambaye
anadai alitungwa jina hilo mwaka 1959 na watoto wenzake kutokana na kucheza
soka ya nguvu akiwa mdogo na mfupi, ambalo limefunika jina lake halisi la
Abdallah Athumani Seif alisema Simba itafanya maajabu ambayo hayakutarajiwa.
"Nina kikosi imara ambacho ni cha
ushindani kilichochanganyika vijana na wakubwa, naamini mchanganyiko utakuwa na
faida kubwa msimu huu," alisema.Kibadeni aliyejiunga na Simba Februari
2, 1969 ikiitwa Sunderland, akitokea Kahe Republic ya Mtaa wa Kongo na
Mchikichi, Kariakoo alisema wamefanya maandalizi ya kutosha na atatoa salamu
katika mchezo wa kwanza dhidi ya Rhino.
Kocha huyo aliyengoza Simba mwaka 1974
kuwa klabu ya kwanza na pekee Tanzania kufika nusu fainali ya Klabu Bingwa
Afrika hadi sasa alisema kama ilivyofanya Manchester, Simba ndiyo itafanya
hivyo.
"Tumeondoka mapema ili tukazoee
mazingira, naamini tutafanya kama ilivyokuwa kwa Man United ambayo ina kocha
mpya kama ilivyo Simba," alisema.
Kocha huyo aliongeza kuwa uwepo wa
wachezaji wapya kama Andrew Ntala, Adeyoum Saleh, Issa Rashid na Betram Mombek,
anaamini watakuwa chachu ya kufanya vizuri msimu huu.
Pia Kibadeni aliyeifunga mabao matatu
peke yake mwaka 1977 katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Yanga, alisema wachezaji
wake wawili waliobaki wakifika timu itazidi kuimarika.
"Bado Tambwe (Hamis) na Kaze
(Gilbert)hawajaripoti katika kikosi changu, viongozi wamenihakikishia
watajiunga na timu hivi karibuni, naamini wakifika Simba itakuwa
imetimia," alisema.
Kocha huyo ambaye mwaka 1993
aliiwezesha Simba SC kufika fainali ya Kombe la CAF akiwa kocha, rekodi ambayo
haijavunjwa hadi leo ikiwa ni miaka 20, aliendelea kusisitiza kuwa mashabiki wa
timu hiyo wala wasiwe na hofu na kikosi chao msimu huu.
Simba ambayo msimu uliopita ilitema
ubingwa ambao ulichukuliwa na watani zao itaanza safari ya kusaka kurejesha
heshima mtaa wa Msimbazi ugenini dhidi ya Rhino ya Tabora ambayo imepanda msimu
huu.
No comments:
Post a Comment