23 August 2013

KEMIKALI ZIWA VICTORIA ZALETA MADHARA KWA VIUMBE NA MAZINGIRAMWANDISHI
Gladness Theonest
‘‘
Hapo baadaye itabidi tutumie teknolojia ambayo itaweza kuondoa sumu iliyopo ziwani kwani itakuwa ni nyingi hivyo wananchi itabidi watumie maji ya visima

PAMOJA n a j u h u d i zinazofanywa na miradi mbalimbali ya mazingira ya kuhakikisha Ziwa Victoria linakuwa salama, bado harakati hizo zimegonga mwamba kutokana na uchafu ambao umekuwa ukitupwa ziwani
. Hatua hiyo inaonesha kuwa, idadi ya watu wanaolitunza ziwa hilo ni ndogo kuliko wanaochafua mazingira. Baadhi ya watu waishio maeneo yanayozunguka ziwa hilo zikiwemo taasisi, hoteli na viwanda, hutupa uchafu mwingi ziwani.
Kutokana na hali hiyo, hivi sasa madhara mbalimbali yameanza kujitokeza kwa binadamu na viumbe hai vilivyomo ziwani. Madhara hayo ni pamoja na mlipuko wa magonjwa kwa binadamu na vifo. Pia kuna sumu nyingi ziwani, kina cha maji na samaki kupungua, kufa na ubora wa maji kubadilika.
MKEMIA AZUNGUMZA
Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Kaimu Meneja wa Maabara ya Ubora wa Maji mkoani Mwanza, Novat Kessy ambaye anasema, pamoja na maji ya ziwa hilo kuendelea kutumika, bado uchafuzi mkubwa unaendelea kufanyika.
Anasema katika ziwa hilo kuna uchafu wa vinyesi vya binadamu na kemikali zinazomwagwa na viwanda vilivyopo jirani na ziwa hivyo kusababisha uwepo wa virutubisho vingi katika maji ambavyo vimechangia kuwepo kwa mimea kwenye maji ijulikanayo kwa jina la kitaalamu "Phytoplankton"
Mimea hiyo ambayo ni midogo, imegawanyika katika makundi mawili, iko yenye rangi ya kijani ambayo ni chakula cha samaki yaani (Phytoplankton Green) na rangi ya bluu ambayo ni sumu kwa samaki (Phytoplankton Blue).
HATARI ILIYOPO
Kessy ambaye ni Mkemia, anasema kutokana na sumu ambazo zinaendelea kuzalishwa ziwani kutokana na virutubisho hivyo, teknolojia inayotumika sasa kutibu maji (water treatment ), haitakuwa na uwezo wa kutibu maji hayo kutokana na uwepo wa vijidudu vingi (sumu), ziwani.
"Tatizo kubwa ambalo linachangia maji yashindwe kutibiwa hapo baadaye ni wingi wa vijidudu vya Phytoplankton, hivi sasa teknolojia inayotumika ni ile ya kuondoa tope na kutibu maji ili kuondoa vijidudu vinavyosababisha magonjwa ya milipuko.
"Hapo baadaye itabidi tutumie teknolojia ambayo itaweza kuondoa sumu iliyopo ziwani kwani itakuwa ni nyingi hivyo wananchi itabidi watumie maji ya visima," anasema.
MADHARA YA SUMU
Kutokana na wingi wa sumu hiyo ziwani, Kessy anasema hali hiyo inachangia viumbe hai kama samaki waliopo ziwani washindwe kuishi kutokana na mimea hiyo kusababisha hewa ya oksijeni kukosekana katika maji.
Anasema ifikapo Machi kila mwaka, samaki wakubwa hufa kwa kukosa oksijeni ambapo kipindi hicho maji huwa yanajichanganya.
"Ile mimea yenye virutubisho inakuwa inaoza kwa sababu ya kuozeshwa na wadudu, baaadaye inakwenda chini na kusababisha bakteria wanaotumia oksijeni...hali hii huchangia oksijeni kupungua ziwani na samaki kufa," anasema Kessy.
Anaongeza kuwa, madhara mengine yanarudi kwa jamii kwani awali gharama ya maji ilikuwa ndogo lakini kutokana na pesa nyingi inayotumika kutibu maji, bili za maji kwa wananchi zitalazimika kupanda kila mwezi.
MAA BARA YA MA J I BUKOBA
Mkuu wa Maabara hiyo, Marco Vita anasema ubora wa maji katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, wakati wa masika unakuwa mbaya zaidi kutokana na watu kutumia mwanya huo kutapisha vinyesi na kulifanya ziwa hilo kuwa chafu.
Anasema kutokana na hali hiyo, wanalazimika kutumia dawa nyingi ya kutibu maji licha ya Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Bukoba (BUWASA), kuweka dawa ya kutibu maji kabla hayajaenda kwa wananchi kwa ajili ya matumizi.
"Dozi wanayoweka BUWASA bado haitoshelezi kutokana na maji hayo kuonekana machafu...hivi sasa magonjwa ya kuharisha, matumbo kwa watoto na watu wazima, yanaongezeka kwa kasi kubwa ambapo wananchi pia hulazimika kuchemsha maji," anasema.
WADAU WA MAZINGIRA BUKOBA
Bw. Michael Cleophans ni mdau wa mazingira na Katibu Mkuu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Envirocomet ambaye anadai kuwa, uchafuzi wa mazingira katika ziwa hilo umeleta madhara mbalimbali katika Manispaa ya Bukoba na maeneo mengineyo.
Anasema kumekuwa na bakteria wengi kwenye samaki ambao huathiri watumiaji samaki na watu wanaokwenda ziwani kuoga kupata magonjwa ya ngozi.
"Vyanzo vingi vya maji vimeendelea kukauka, ukilinganisha na miaka 10 iliyopita, kina cha maji katika ziwa hili kimepungua kwa mita mbili... hivi sasa ziwa limebaki na aina tatu tu za samaki ambao ni sato, sangara na dagaa.
"Pamoja na kuwepo kwa samaki hawa, pia wingi wao umepungua ziwani ambapo kipindi cha miaka 10 iliyopita, zilikuwa zinavuliwa tani 750 za samaki lakini kwa sasa zinavuliwa tani 350 tu.
Bw. Cleophans anasema, uvuvi haramu umekuwa mkubwa kuliko utunzaji wa ziwa na samaki ambapo taka ngumu zimekuwa zikimwagwa ziwani na kuwa chakula cha samaki.
WANANCHI WA KAWAIDA
Bw. Thomas Ngaiza ambaye ni mkazi wa Mji wa Bukoba, anasema kutokana na uchafu wa mazingira uliopo katika ziwa hilo, hivi sasa kuna magonjwa mengi ya milipuko hospitalini ukiwemo wa tumbo (typhod), ambayo awali hayakuwepo.
Anasema maji yanayotumiwa na wananchi majumbani ambayo hutibiwa na BUWASA yamekuwa machafu sana pamoja na ongezeko la magonjwa ya ngozi.
KAIMU MGANGA MKUU
Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Bukoba, Dkt. Martin Muganyizi, alipohojiwa kuhusu magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji ya ziwa hilo kwa wananchi, alisema kwa sasa yamekuwa mengi.
Anasema mwaka 2011/2013, magonjwa yaliyoripotiwa ni pamoja na kuhara, homa za matumbo ambayo ilionekana kuwashambulia watu wengi zaidi kutokana na matumizi ya maji hayo na magonjwa ya ngozi.
Anaongeza kuwa, kundi ambalo linaathirika zaidi kutokana na magonjwa hayo ni watoto na wazee ambao uharisha ambapo vijana na wazee pia huathirika zaidi na magonjwa ya ngozi.
TAKWIMU ZA MAGONJWA
Dkt. Muganyizi anasema, katika kipindi cha mwaka 2011-13, jumla ya kesi 12,556 za magonjwa ya kuharisha zilizolipotiwa zikijumuisha watoto walio chini ya miaka mitano na zaidi.
"Wanaume walikuwa 5,708, wanawake 6,848, katika magonjwa ya ngozi kulikuwa na kesi 4,643 ambazo ziliripotiwa katika kipindi hicho wakiwemo wanaume 2,399, wanawake 2,244," anasema.
VIFO VILIVYOTOKEA
Dkt. Muganyizi anasema, vifo vilivyoripotiwa katika kipindi cha mwaka 2011-12 kwa ugonjwa wa kuharisha pekee wagonjwa 42 walipoteza maisha (chini ya miaka mitano na zaidi), kati ya hao, wanaume 29, wanawake 13.
JAMII IFANYE NINI
Ili kuepuka vifo na madhara mengine yatokanayo na matumizi ya maji katika ziwa hilo, Dkt. Muganyizi anasema jamii inapaswa kunywa maji yaliyo safi na salama yaliyochemshwa na kutibiwa, matumizi sahihi ya vyoo, kuosha matunda kabla ya kula, kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kabla ya kula, kutoka chooni.
Aliitaka BUWASA iboreshe huduma za usambazaji maji safi kwa wananchi na kuishauri jamii, viwanda, hoteli na taasisi kuhakikisha shughuli zao hazichafui mazingira ya ziwa hilo ambalo lina msaada na mchango mkubwa kwa wananchi na Taifa.
U t a f i t i wa makala h i i umefadhiliwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF).

No comments:

Post a Comment