Na Mwajuma Juma,
Zanzibar
KINYWAJI kisicho na kilevi cha Grand
Malt, ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu ya Zanzibar maarufu kama 'Grand Malt
Premier League' jana wamekabidhi vifaa kwa timu 12 zinazoshiriki ligi hiyo
katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Bwawani, mjini hapa.
Mbali na
kumwaga vifaa hivyo, Grand Malt pia wameongeza udhamini wao kwa waamuzi na
uendeshaji wa ligi, ambapo msimu huu watatoa kiasi cha Sh milioni 200 kutoka
sh. milioni 140 za msimu uliopita.Hafla hiyo
maalumu ya kukabidhi vifaa na kutangaza kiasi hicho kipya cha uendeshaji wa
ligi, ilihudhuriwa na viongozi na wanamichezo mbalimbali wakiongozwa na Waziri
wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ), Saidi Ali Mbarouk.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbarouk
alisema wamefurahishwa mno na Grand Malt kwa kuongeza udhamini wao pamoja na
kutoa vifaa bora vya michezo kwa timu zote zishiriki."Tuna uhakika sasa soka ndani ya
Zanzibar itazidi kusonga mbele, ombi lenu kwenu ZFA (Chama cha Soka Zanzibar),
pamoja na wadau wote kutumia fursa hii kuhakikisha tunafika kule tunakokutaka.
"Nawasifu zaidi Grand Malt kwa
kuendelea kudhamini Ligi Kuu ya Zanzibar na hii inadhihirisha tuko nao pamoja
kwa mambo mengi, nasi pia tunapaswa kuwaunga mkono kwa kutumia kinywaji
chao," alisema.Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Grand
Malt, Kushillah Thomas alisema, kinywaji hicho kitaendelea kushirikiana na watu
wa Zanzibar katika kuhakikisha wanafanikiwa kwenye malengo yao.
"Udhamini huu ni mwanzo tu na
tunaamini utasaidia kwa kiwango kikubwa kufanikisha malengo ya soka ya
Zanzibar," alisema.Viongozi wa ZFA nao walikiri
kufurahishwa na udhamini huo na kusema, wanaamini Ligi Kuu ya Grand Malt msimu
huu itakuwa na ushindani mkubwa zaidi.
KMKM ndio waliofanikiwa kutwaa ubingwa
huo msimu uliopita, wakiwa ni mabingwa wa kwanza toka kuanza kwa udhamini wa
Grand Malt.
Mbali na KMKM timu nyingine
zinazoshiriki ligi hiyo ni Fuoni, Chuoni, Polisi, Malindi (Bandari), Zimamoto,
Mafunzo, Jamhuri, Chipukizi, Kizimbani, Mtende na Miembeni.
No comments:
Post a Comment