Na Mwandishi Maalun
RAIS Mstaafu wa 42 wa Marekani, Bill
Clinton, amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivua ukweli kuwa wana
Serikali ambayo inaongoza kwa kila ubunifu wa kuboresha kila lililo jema kwa
ajili ya wananchi kwa nia ya kujaribu kubadilisha maisha yao kuwa bora zaidi.Aidha, Rais Clinton amesema kuwa kama
taasisi yake ya Clinton Fondation kupitia Mradi wake wa Maendeleo wa Clinton
Development Initiative (CDI) itashindwa kuhakikisha kuwa mradi wake wa kilimo
ambao inauanzisha nchini unakuwa endelevu, basi Clinton Foundation yenyewe
itakuwa imeshindwa.
Rais Clinton aliyasema hayo juzi, Ikulu,
Dar es Salaa
m, wakati alipozungumza kwenye sherehe ya kutiwa saini kwa
makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Clinton Foundation,
ambako taasisi hiyo itasaidia maendeleo ya kilimo na wakulima wadogo wadogo kwa
kuboresha kilimo chao, kiwango chao cha mazao, ubora wa mazao yenyewe na hivyo
kuinua kipato chao.
Mara baada ya Rais Clinton na mwenyeji
wake Rais Jakaya Kikwete, kuwa wameshuhudia kutiwa saini kwa makubaliano hayo,
Rais Clinton aliwaambia waliohudhuria hafla hiyo wakulima 10 kutoka mkoa wa
Iringa na waandishi wa habari kuwa;
"Makubaliano haya ni mfano mwingine
wa jitihada za Serikali ya Tanzania kuboresha maisha ya watu wake. Kwa hakika,
watu wa nchi hii lazima watembee kifua wazi na wanayo kila sababu ya kujivunia
ukweli kuwa Serikali yao inaongoza katika kila ubunifu wa kuboresha kila lililo
jema kwa ajili ya wananchi kwa nia ya kuboresha maisha yao."
Mapema marais hao wawili walikutana na
kuzungumza na wakulima wadogo wadogo 10 kutoka Mkoa wa Iringa, ambako CDI
imeanza shughuli zake katika kilimo na ambako makubaliano yaliyotiwa saini juzi
yataelekeza nguvu zake.
Alisema chini ya mradi huo litaanzishwa
shamba la mfano kwa ajili ya wakulima kuona mbinu mpya na bora za kilimo, kutoa
mafunzo na kushiriki uzalishaji.
Alisema kuwa mashamba ya namna hiyo
yamefanikiwa sana katika nchi nyingine za Afrika ambako CDI inaendesha shughuli
zake ikiwamo Malawi.
"Katika Malawi tulianza na shamba
moja na sasa kuna mashamba ya mfano 21 ambayo yamekuza kipato cha wakulima mara
tano na kuongeza uzalishaji mara mbili unusu,"alisema.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, Rais Kikwete ameisifu Taasisi ya Clinton Foundation kwa
mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Tanzania katika miaka 10 ambayo taasisi
hiyo imekuwepo Tanzania na hasa katika nyanja za afya na sasa kilimo.
No comments:
Post a Comment