05 August 2013

WANAFUNZI 8000 WAKWAMA KUJIUNGA VYUO VIKUU NCHINI


 Na Hussein Makame, Maelezo
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imekataa majina ya wanafunzi 8,805 walioomba kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kutokana na sababu mbalimbali zilizojitokeza kwenye fomu za waombaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Sifuni Mchome, wanafunzi hao hawakuchaguliwa na tume hiyo kujiunga na vyuo vikuu kutokana na maombi yao ya programu zote walizochagua kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa sababu za kutochaguliwa kwa wanafunzi hao ni pamoja na ushindani wa wanafunzi katika programu walizochagua, wanafunzi kushindwa kuwasilisha programu walizochagua na kuchagua programu ambazo hawana sifa nazo.
Hata hivyo, TCU imesema inawapa nafasi nyingine wanafunzi hao kuomba tena kwa awamu ya pili kwa kuchagua programu nyingine ambazo wana sifa nazo kupitia mfumo wa udahili wa TCU, ambao umeshafunguliwa tangu Julai 29 hadi Agosti 9, mwaka huu, utakapofungwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanafunzi anatakiwa kuangalia jina lake katika orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa na TCU, orodha inayopatikana kwenye tovuti ya taasisi hiyo.
"Ba a d a y a mwa n a f u n z i kuthibitisha jina lake kwenye orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa iliyoko kwenye tovuti ya TCU, unatakiwa kufuata masharti yafuatayo, chagua programu moja tu kutoka kwenye orodha ya programu inayopatikana kwenye tovuti ya TCU," ilisisitiza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa masharti hayo, pia mwanafunzi anatakiwa kufungua mwongozo wa udahili unaopatikana kwenye tovuti hiyo na kuthibitisha kwamba anayo sifa stahiki ya kujiunga na programu aliyoichagua.

1 comment:

  1. umakini unahitajika wakati wa kuomba vyuo, si kila credits za masomo zinafit kuomba course yoyote vyuoni. huwezi kuwa na pass za HGL then ukaomba medicine eti kwa sababu kuna fursa ya kuomba kozi zaidi ya moja.

    ReplyDelete