- UONGOZI 'WAANGUA KILIO' TFF
Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts
amemtupia lawama mwamuzi wa mechi Ligi Kuu kati ya timu yake na Coastal Union
juzi, Martin Saanya kwa kushindwa kumudu mchezo huo na kutoa maamuzi yenye
utata.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.Akizungumza Dar es Salaam juzi mara
baada ya mchezo huo kumalizika, Brandts alisema ameshangazwa na maamuzi ya
mwamuzi huyo, mbaya zaidi akawapa penalti wapinzani wao iliyojaa utata, kwa madai
hakuna mchezaji wake aliyeunawa mpira eneo la hatari.
"Mwamuzi amechangia kutunyima
pointi tatu katika mchezo ule, maamuzi yake yalijaa utata mtupu sasa ile
penalti aliyowapa Coastal, hata haijulikani ni kwa sababu gani kwa kuwa hakuna
mchezaji wangu ambaye aliunawa mpira," alisema Brandts.Alisema pia ilishangaza watu wengi
baada ya mchezaji wake, Simon Msuva kupewa kadi nyekundu na wakati alifanyiwa
madhambi na Abdi Banda wa Coastal, lakini akampa kadi mchezaji ambaye
hakuhusika na ugomvi Chrispine Odula.
Brandts alisema wanasubiri ripoti ya
Kamisaa wa mchezo huo itakapotoka kama kweli alikuwa makini atabaini madudu ya
mwamuzi huyo, ambaye tangu kuanza kwa mchezo alionekana kushindwa kuumudu
mpambano huo.Alisema hali hii ikiendelea kwa waamuzi
kushindwa kumudu michezo inayoendelea, bingwa atashindwa kupatikana kwa njia
halali na badala yake, atapatikana kwa kubebwa na waamuzi.
Hata hivyo mara baada ya mchezo huo
vurugu kubwa ziliibuka kwa mashabiki wa Yanga, ambao walikuwa wakitaka kumpiga
mwamuzi huyo kutokana na maamuzi yake.Lakini askari ilibidi watumie maji ya
kuwasha, ili kuwatawanya mashabiki hao ambao hata hivyo walikwenda kumsubiria
nje.
Katika hatua
nyingine, uongozi wa klabu hiyo umepeleka barua Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), wakitaka kadi nyekundu aliyooneshwa mchezaji Simon Msuva ifutwe
na mwamuzi Saanya aadhibiwe.
No comments:
Post a Comment