29 August 2013

AJALI YAUA 13

  • WENGINE 11 HOI,WAVUNJIKA MIKONO,NYONGA


Suleiman Abeid, Shinyanga na Faida Muyumba, Geita
WATU 13 wamekufa na wengine 11 kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyotokea saa 2.30 usiku wa kuamkia jana baada ya gari dogo aina ya Hiace kugonga kwa nyuma gari aina ya Scania lililokuwa limeharibika na kuegeshwa pembeni mwa barabara.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kihenya Kihenya, alisema ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Ngogwa wilayani Kahama wakati gari hilo dogo la abiria namba T. 756 CHX likitokea mjini Kahama kwenda katika mji wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoa wa Geita.Alisema lilipofika eneo hilo ndipo lilipogonga kwa nyuma lori hilo namba T. 999 AMS.
  Kihenya alisema kuwa katika ajali hiyo jumla ya watu 11 walifariki eneo la ajali akiwemo mtoto mchanga wa miezi saba. Aliongeza kuwa wengine wawili walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Serikali wilayani Kahama.Kamanda huyo alisema mpaka jana mchana maiti saba zilikuwa zimetambuliwa ambao ni pamoja na mtoto mwenye umri wa miaka saba aliyetambuliwa kwa jina la Kasandu Jumanne mkazi wa Mwanza, Masanja Matogolo (Kahama) na David Charles (Masumbwe, Bukombe).
 Wengine waliotambuliwa jana ni Regina John (Rorya), Ezekiel Mnyiko, ambaye alikuwa dereva wa Hiace na Peter Daud (wote wakazi wa Ushirombo) na Mlekwa Mguhati (Masumbwe).Kihenya alisema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. Hata hivyo alisema huenda ilisababishwa na mwendo kasi na uzembe wa dereva kutokuwa makini barabarani.
 Alisema hali za majeruhi ni mbaya na taratibu zilikuwa zinafanyika ili kuwahamishia Hospitali ya RufaaBugando mkoani Mwanza, huku majeruhi 9 hali zao zikiendelea vizuri. Al i s ema ma j e r u h i we n g i wamevunjika mikono na nyonga.Kwa upande mwingine Kaimu Kamanda huyo aliwashukuru wakazi wa Kijiji cha Ngongwa kutokana na ushirikiano wao waliouonesha kwa jeshi hilo mara baada ya kutokea ajali hiyo na kutoa mwito kwa wananchi kufika katika hospitali ya serikali mjini Kahama ili kuweza kutambua maiti zilizohifadhiwa katika hospitali hiyo. 

No comments:

Post a Comment