26 July 2013

YANGA YALAMBA KIFAA KIPYA



Na Elizabeth Mayemba
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Javu tayari amemwaga wino katika klabu kongwe nchini ya Yanga na moja kwa moja jana alianza mazoezi na wenzake Uwanja wa Loyola Mabibo, Dar es Salaam.Javu amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu hiyo ambao pia ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Abdallah Bin Kleb alisema wamemalizana na Javu pamoja na klabu yake ya Mtibwa na sasa ni mchezaji mpya wa Jangwani."Tumemsainisha Javu miaka miwili, tumemalizana naye yeye na klabu yake," alisema Bin Kleb.
Klabu hiyo imeamua kumsajili Javu ili kuimarisha safu ya ushambuliaji baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo kumfungashia virago Mnigeria Ogbu Brendan Chukwudi.
Pia Javu aliwahi kuwa mchezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati timu hiyo ilipokuwa ikinolewa na Mbrazil Marcio Maximo.Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwani sasa inakuwa na watu wanne, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Shaaban Kondo.
Javu ni mchjezaji wa tatu kutoka katika timu yake ya Mtibwa kusajiliwa kwani tayari Yanga ilimnasa beki, Rajab Zahir huku mahasimu wao Simba wakimsajili Issa Rashid 'Baba Ubaya' na Shaaban Kisiga alijiondoa mwenyewe baada ya kutofautiana na kocha wake.

No comments:

Post a Comment