Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Taifa, Taifa Stars imewasili
salama mjini Kampala, Uganda tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya
Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa
Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.Stars ambayo
iliwasili Kampala juzi ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku
10 kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili
itakwenda Afrika Kusini mwakani, imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la
Kisseka katikati ya Jiji la Kampala
Kocha Mkuu wa
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen
ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania
Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala
kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Stars ambayo
ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa
Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi
yake ya mwisho leo Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya kesho.
Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni
ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako
vizuri na ari kwa ajili ya mechi hiyo.Wachezaji wote wapo katika hali nzuri,
isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa
madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.
Kikosi kamili cha Stars kilichoko
Kampala kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni
Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na
Vincent Barnabas.
Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd,
Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na
Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.
Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na
waandishi wa habari Jumatatu ijayo Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi
katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment