Na Mwandishi Wetu, Tanga
SERIKALI imeshauriwa
kuwachukulia hatua kali wamiliki wa kumbi za starehe wanaowaruhusu watoto wenye
umri chini ya miaka 18 kuingia katika maeneo hayo kwani kufanya hivyo ni
kuvunja sheria na ukiukwaji wa haki za mtoto.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Tanga jana, Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA)
mkoani Tanga, Yona Lucas kila mmoja anatakiwa kutekeleza sheria hiyo na kwamba
kitendo cha kumruhusu mtoto kuingia katika kumbi za starehe ni ukiukwaji wa
haki ya mtoto ya kupata malezi bora.
Lucas alisema katika siku za hivi karibuni
imeonekana ni kitu cha kawaida kuona watoto wadogo wanaingia katika kumbi za
starehe huku wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia bila wao kujijua
na wamiliki wa maeneo hayo wakifurahia kupata fedha kutokana na uwepo wa watu
hao.
Alisema wanaohusika kufanya makosa hayo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali
kwani kwa kuwaachia ni sawa na kuwanyima haki watoto ambao wanatakiwa kukua
katika misingi ya maadili. Hata hivyo, alisema Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009
inakataza mtoto chini ya miaka 18 kufanyiwa vitendo vitakavovunja haki zako,
huku sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu mtoto wa kike kuolewa kwa idhini ya
mzazi akiwa na miaka 14 na kwamba kunaonekana kukinzana kwa sheria hizo.
Aliwataka Watanzania kupitia mabaraza ya katiba kutoa hoja zitakazopelekea katiba
kutoa suluhu katika mgongano wa sheria za mtoto ,kwa kufanya hivyo kunaweza
kumsaidia mtoto kukua bila kugudhiwa na vitendo vya ukiukwaji wa sheria.
No comments:
Post a Comment