23 July 2013

WANANCHI WAPINGA SERIKALI TATUNa Suleiman Abeid, Simiyu

WAKAZI wa Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na changamoto nyingi zilizomo ndani ya rasimu ya katiba na kwamba zinapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kina kabla ya kuandikwa rasmi kuwa Katiba Mpya nchini.
Wakitoa maoni yao katika mdahalo ulioandaliwa na Muungano wa asasi za kiraia wilayani Maswa (MASWANGONET) kwa ufadhili wa The Foundation For Civil Society uliofanyika juzi wakazi hao walisema yapo maeneo mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho kabla ya rasimu hiyo kufikishwa katika bunge la katiba.

Baadhi ya eneo lililotajwa kuwa na changamoto nyingi ni suala la muundo wa Muungano iwapo muundo wa Serikali tatu utakubalika na kwamba haieleweki ni jinsi gani itifaki ya marais wa Tanzania Bara, Serikali ya Zanzibar na yule ya Muungano itakavyoweza kutekelezwa.

Walisema rasimu ya hivi sasa haielezi kwa kina suala la itifaki za watakaokuwa marais chini ya muundo wa Serikali tatu na kuhoji iwapo Rais wa Muungano amehudhuria sherehe ya kitaifa katika nchi moja washiriki wa muungano ni rais yupi anayepaswa kutangulia katika uwanja wa sherehe na kupigia mizinga ya heshima kama ikibidi kupigwa.

"Kwa kweli rasimu yetu bado ina maeneo mengi sana yanayopaswa kufanyiwa marekebisho na kupatiwa ufafanuzi wa kina, binafsi ninapata wasiwasi sana katika suala zima la itifaki ya marais wetu itakuwaje, sasa lifanyiwe kazi kwanza suala hilo ndipo tutoe maoni yetu."

"Mfano ni hali halisi inavyotokea kule visiwani wakati Rais wa Muungano anapokaribishwa katika sherehe mbalimbali za kitaifa mfano sherehe za mapinduzi, tunaona yeye ndiye anayetanguliwa uwanjani, kisha mwisho ndipo anaingia Rais wa Serikali ya Mapinduzi, hapa kuna mkanganyiko, kwa kawaida Rais wa Muungano ndiye anapaswa kuingia mwisho," alieleza Ezekiel Kassanga.

Hata hivyo, washiriki wa mdahalo huo walikubaliana kuwepo kwa muundo wa serikali tatu nchini na pia kushauri kutumika kwa jina la Serikali ya watu wa Tanganyika badala ya Tanzania bara na kwamba kutotambuliwa kwa Tanganyika kutasababisha kupotea kwa jina hilo ambalo ni moja ya washiriki wa muungano huo.
Mbali ya kupotea kwa jina hilo pia washiriki hao walionesha wasiwasi kwamba kutamkwa kwa neno Tanzania Bara inaweza kusababisha kutokea kwa mgogoro mkubwa siku zijazo kwa baadhi ya maeneo ya Tanganyika ambayo ni visiwa kuamua kujitenga kwa vile hayatajwi ndani ya katiba kuwa ni sehemu ya Tanganyika

1 comment:

  1. kwa kweli wananchi tuliowengi hatutaipigia kura ya maoni katiba mpya endapo suala la serikali tatu kutokuwepo.Hakuna asiyefahamu urasimu uliojaa kwenye muungano wa sasa ambapo nchi moja imekuwa ikikandamizwa kwa muda mrefu.Wanzibari watajitenga tu.......

    ReplyDelete