23 July 2013

JK APONGEZWA KUANZISHA MIKOA MIPYA



 Na Suleiman Abeid, Simiyu

MBUNGE wa Jimbo la Busega wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu, Dkt. Titus Kamani amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukubali kwake kuundwa kwa Mkoa mpya wa Simiyu hali ambayo imewezesha kusogezwa karibu zaidi kwa huduma za jamii kwa wakazi wa jimbo la Busega. Dkt. Kamani alitoa pongezi hizo katika uzinduzi rasmi wa Halmashauri mpya ya Wilaya ya Busega mwishoni mwa wiki iliyopita iliyokuwa awali chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza ambapo alisema kuanzishwa kwa maeneo mapya kunasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akizungumza katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo, mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu alisema kuanza kazi kwa Halmashauri ya Busega kutaharakisha maamuzi katika kuwahudumia wananchi na kuwataka madiwani kushirikiana pamoja katika kufanya kazi zao.

"Binafsi ninayo furaha kubwa kuona jimbo letu la Busega limepata halmashauri yake, nieleze wazi kuwa anayestahili pongezi nyingi ni Rais wetu Jakaya Kikwete, hatua yake ya kuruhusu uanzishwaji wa maeneo mapya nchini imesaidia kusogeza karibu zaidi huduma za kijamii kwa wananchi wake." "Kazi iliyoko mbele yetu hivi sasa ni wananchi wa Busega kushirikiana na wawakilishi wao (madiwani) katika kuhakikisha tunafanya kazi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa bidii, na ndugu zangu madiwani shikamaneni na kufanya kazi kama timu moja imara," alisema Dkt. Kamani.


Wakati huo huo madiwani wa halmashauri hiyo walimchagua Charles Lukale diwani wa kata ya Igalukilo kuwa mwenyekiti wa kwanza wa halmashauri baada ya kupata kura zote 17 zilizopigwa ambapo Ng'habi Moja kutoka Kata ya Kalemela alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.

Wenyeviti wengine wa kamati za kudumu waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Vumi Magoti kutoka kata ya Kiloleli anayekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu na Maji na Maridadi Ntobi atakayeongoza Kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira.
Wilaya mpya ya Busega ilianzishwa baada ya kutenganishwa kwa majimbo mawili ya Magu na Busega wilayani Magu Mkoa wa Mwanza ambapo katika kuundwa kwa Mkoa mpya wa Simiyu Wilaya ya Busega iliunganishwa na Wilaya za Bariadi, Itilima (mpya), Maswa na Meatu zilizokuwa sehemu ya Mkoa wa Shinyanga

No comments:

Post a Comment