Na Jovin Mihambi, Mwanza
WAKAGUZI wa Ndani wa Serikali wametakiwa
kuandaa taarifa zao kwa wakati na kuzipeleka kwenye taasisi husika hali ambayo
itasaidia kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara katika baadhi ya kumbukumbu za
hesabu katika ofisi za Serikali.
Hayo yalielezwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu
wa Serikali, Chotto Sendo wakati wa ufunguzi wa semina ya wastahiki meya,
wenyeviti wa kamati za ukaguzi na wakaguzi wa ndani wa halmashauri za majiji,
manispaa, wilaya na miji, kanda ya ziwa iliyofanyika jijini humo.
Alisema kuwa uandaaji wa taarifa mapema na
kuziwasilisha kwa wakati katika ngazi zinazohusika pia ni kuwajengea uwezo
wakaguzi wa ndani na wadau wa ukaguzi wa ndani kwa kuimarisha miundombinu ya
ukaguzi na kupunguza hati zenye mashaka na baadaye kupata ofisi zote za
Serikali nchini kuweza kupata hati safi.
Naye mratibu wa semina hiyo, Enock Mayage
alisema kuwa katika mafunzo hayo, washiriki wapatao 100 kutoka Mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Mara na Simiyu, watapata fursa ya kujadili kwa uwazi changamoto
zinazowakabili katika ukaguzi wa ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na
kuzitafutia mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kuondokana nazo kwa kutumia
rasilimali zilizopo.
Aidha, alisema semina kama hiyo ilishafanyika katika Kanda ya Nyanda za
Juu (Mbeya) Kanda ya Kati (Dodoma) na Kaskazini (Arusha) na kujumuisha
washiriki 243 na kuongeza hadi mwisho wa semina hiyo itakuwa imehusisha
washiriki 343 na kuongeza kuwa semina nyingine itafanyika katika Kanda ya Mashariki
(Dar es Salaam)
No comments:
Post a Comment