Na Moses Mabula, Tabora
WATU watano
wanaodhaniwa kuwa majambazi wamemuua mfanyabiashara mmoja kwa kumpiga risasi
tumboni katika Kijiji cha Nsungwa wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Tukio hilo
limetokea hivi karibuni ambapo majambazi hao wenye silaha za kivita waliteka
kijiji hicho kisha kupora mali mbalimbali katika maduka ya wafanyabiashara wa
kijiji hicho cha Nsungwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Peter
Ouma alisema kwamba majambazi hao walimuua January Robert na kuiba vitu mbalimbali
vya dukani pamoja na fedha taslimu shilingi 370,000 kisha kutoroka.
Alisema kuwa marehemu Robert aliuawa
wakati akijaribu kutoa msaada wa kuzuia wizi huo usifanyike katika maduka hayo
ndipo watu hao wakamfyatulia risasi tumboni na kufariki dunia papo hapo.
Kamanda Ouma alisema mara baada ya tukio
hilo polisi ilifanya msako mkali na kufanikiwa kumpata mtuhumiwa mmoja Bahati
Masanja ambaye inadaiwa kuwa ni miongoni mwa waliofanya mauaji ya
mfanyabiashara huyo.
Alisema kwamba watu hao wanaodaiwa kuwa
watano walivamia Kijiji hicho na kuvunja vibanda vitatu vya biashara na kuiba
vitenge, vitambaa, vocha zenye thamani ya shilingi 40,000 na fedha taslimu
kiasi hicho na kisha kukimbilia kusikojulikana.
Hata hivyo aliwataka wananchi Mkoa wa
Tabora kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikiwa
kukamatwa kwa watu hao kwani "watu hao tunaishi nao ni majirani
zetu."alisema.
No comments:
Post a Comment