Na Grace Ndossa
SHIRIKA lisilokuwa la
kiserikali la Ujerumani (GLRA), limekabidhi magari mawili na pikipiki 10 kwa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kusaidia waratibu wa kifua kikuu
na ukoma waweze kuwafikia walengwa sehemu walipo kwa muda mwafaka.
Akikabidhi
magari hayo mwakilishi wa shirika hilo GLRA kwa upande wa Tanzania Burchard
Rwamtonga alisema kuwa magari hayo pamoja na pikipiki yana thamani ya sh.
milioni 124 kwa ajili ya kitengo cha kudhibiti kifua kikuu na ukoma kilicho
chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili kupata huduma kwa wakati.
Pia alisema
kuwa shirika hilo linakabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa upatikanaji wa
msamaha wa kodi na VAT kwa magari, pikipiki na vipuri vinavyoingizwa nchini kwa
ajili ya matumizi ya mpango wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma.
Alisema kuwa
magari pamoja na pikipiki zilizotolewa ziliingizwa nchini Desemba 2011, shirika
lilipata kibali cha msamaha wa kodi na kutoa magari na pikipiki Desemba mwaka
2012, hivyo vifaa hivyo vilikaa bandarini kwa muda wa mwaka mmoja na kugharimu
shirika sh. milioni 13 kama gharama za matunzo.
Naye Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashidi alisema kuwa wametoa
msaada kwa wakati mwafaka ili kubadilisha magari na pikipiki zilizochakaa.
Pia alitoa agizo kwa watumiaji wa vyombo hivyo
katika mikoa yote Tanzania kuyatunza magari pamoja na pikipiki ili yaweze kuwa
katika hali nzuri na hivyo kuweza kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi
No comments:
Post a Comment