Na Grace Ndossa
BARAZA la Vyuo Vikuu
la Afrika Mashariki (IUCEA), linafanya tafiti katika nchi tano za Afrika
Mashariki kuangalia ubunifu na uwezo walionao wanafunzi pamoja na changamoto
zilizopo katika elimu ya vyuo vikuu katika kupata ajira.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mtendaji wa
baraza hilo, Profesa Mayunga Nkunya alipokuwa anazungumza na waandishi wa
habari kuhusu kongamano litakalofanyika Nairobi na kuunganisha Baraza la
wafanyabiashara la Afrika Mashariki (EABC) na kujadili ni wanafunzi wenye sifa
gani wanaotakiwa katika soko la ajira.
Alisema kuwa utafiti huo unafanyika kwa miezi mitatu na kuweza
kujadili katika kongamano hilo ambalo litajumuisha wafanyabiashara wa Afrika
Mashariki ni vipaji gani walivyokutana navyo katika elimu ya juu na ubunifu ili
kueleza wafanyabiashara hao.
Alisema kuwa hii ni kutokana na vijana wengi wanamaliza shule
hawana ajira wanabaki mitaani, kutokana na elimu wanayoipata hivyo, mfumo wa
elimu unatakiwa uendane na kile ambacho anaenda kufanya katika eneo la kazi.
"Kongamano hilo litajadili na kufahamu wafanyabiashara
wanahitaji watu wa namna gani au wanafunzi wenye sifa gani katika nafasi za
ajira kwani kwa Tanzania fursa nyingi zinachukuliwa na wageni kutokana na
wanafunzi wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu hawana ujuzi unaotakiwa sokoni,"
alisema Profesa Nkunya.
Alisema kuwa washiriki watakuwa ni vyuo vya elimu ya juu,
wafanyabiashara wa Afrika Mashariki, pamoja na washiriki mbalimbali ili
kujadili ni wanafunzi wa namna gani wanaohitajika kwenye soko la ajira.
Hata hivyo alisema kuwa katika mkutano huo watajadili ni vitu gani
vinatakiwa kufanyiwa maboresho na kujadili changamoto zilizopo katika elimu ya
vyuo vikuu.
Profesa Nkunya alisema kuwa kwa
sasa wanaangalia utaratibu ambao utakuwa unaangalia uwezo wa kila mwanafunzi
ili kila mmoja aweze kwenda chuo kikuu badala ya kumpima mtu kwa kutumia
mitihani.
No comments:
Post a Comment