Na Leah Daudi
SERIKALI imepiga marufuku unywaji wa pombe muda wa kazi wilayani Rombo
mkoani Kilimanjaro hali hiyo imeelezwa kuchangia utengenezaji na unywaji zaidi
wa pombe za kienyeji ikiwemo gongo. Serikali
wilayani humo inazuia unywaji wa pombe hadi saa 9:00 alasiri kwa pombe zote,
licha ya kufanikiwa kwa operesheni hiyo lakini inaelezwa kulegalega kwenye
pombe za kienyeji na kuchangia kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Wananchi
ambao walizungumza na gazeti hili kwenye Kata za Mashati, Tarakea na Mkuu
walisema kuwa askari wamekuwa wakizunguka kwenye maeneo yanayouza vileo kama
bia na pombe kali pekee, huku wakishindwa kabisa kudhibiti uuzaji wa pombe za
kienyeji na unywaji ukiongezeka. Mmoja
wa mwananchi ambaye anafanya biashara ya vileo, Prediganda Marandu alisema kuwa
askari wamekuwa wakitoza faini watu wanaokunywa pombe muda wa kazi lakini
wamekuwa hawatoi risiti kwa faini wanazotoza.
"Wakija
wakikuta mtu anakunywa bia wanataka shilingi 50,000 na anayekunywa anatozwa
faini lakini cha kushangaza ni kwamba risiti hawatoi, lakini wananitoza faini
hapa nyuma yangu kuna watengenezaji wa gongo lakini hawaendi kuwakamata,"
alisema. Baadhi
ya wananchi ambao hawakutaka majina yao yataje hapa walisema kuwa operesheni
hiyo ya kukamata watu wanaokunywa pombe muda wa kazi ni nzuri ila tatizo
imegeuka mradi kwa baadhi ya Polisi na watendaji waliopewa jukumu hilo.
Mkuu wa
Wilaya ya Rombo, Elinasi Pallangyo alisema kuwa malalamiko yanayoelezwa na wananchi
juu ya polisi kuomba rushwa hawezi kukataa kwani baadhi ya polisi wamekuwa siyo
waaminifu, hivyo kusababisha mazingira magumu katika utekelezaji wa operesheni
hiyo.
Gazeti
hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Robert Boaz kuzungumzia askari
wake kulalamikiwa kuhusika na vitendo vya rushwa ambapo alisema malalamiko hayo
hayajamfikia ila anataarifa za operesheni inayoendelea wilayani Rombo ya
kuwakamata watu wanaokunywa pombe muda wa kazi ikiwemo pombe za kienyeji. Alisema kama
wananchi wana ushahidi wa kutosha juu ya Polisi kuhusika katika rushwa basi
wajitokeze ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kabisa tofauti na ilivyo hivi sasa
ambapo bado operesheni inaendelea.
No comments:
Post a Comment