04 July 2013

URAIS 2015 SASA MOTO


 Na Yusuph Mussa, Korogwe
KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Bw. Nicholaus Mgaya, amewataka wafanyakazi wote nchini kuungana na shirikisho hilo ili kutoka na msimamo wa kumchagua rais wa awamu ya tano mwaka 2015.
Alisema muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini, siku zote ndio unaochagua rais wa nchi hiyo; hivyo kama wafanyakazi wote wataungana na TUCTA, wataweza kuchagua rais wamtakaye ili matatizo yao yaweze kutatuliwa.
Bw. Mgaya aliyasema hayojana katika warsha ya siku nne inayofanyika mjini Korogwe, mkoani Tanga ambapo unahusisha wawakilishi wa wafanyakazi katika wilaya zote mkoani humo.
"Kabla ya kupiga kura, wagombea wote wa nafasi ya urais tutawaita na kuwapa masharti juu ya kiongozi tumtakaye, nguvu ya chama ni wanachama ambao tukiwa wengi, tuna uwezo wa kumchagua rais ajaye kama ilivyo Afrika ya Kusini," alisema.
Aliongeza kuwa, kwa sasa kuna utitiri wa vyama vya wafanyakazi, vingine vikiwa kwenye mikoba hivyo kama wanataka kupambana na Serikali ili kutetea masilahi yao lazima waungane.
"Kwa sasa tuna vyama 30 vya wafanyakazi, bado kuna vingine vipo kwenye mikoba...ni vyema msajili wa vyama akaliangalia hili maana chama kina miaka mitano, lakini hakina usajili.
"Wafanyakazi wanapinga Rasimu ya Katiba Mpya na kusema haijaweka vitu vingi vinavyowahusu wafanyakazi kama mgomo, lakini kwa vile tumepewa fursa ya kuijadili rasimu husika basi wafanyakazi wote wahudhurie mikutano ili kuipinga," alisema.
 Bw. Mgaya alisema ikiwezekana wafanyakazi wafanye hata maandamano kama katiba hiyo haitaingiza mgomo badala yake limeingizwa suala la Serikali tatu.
Alisema mgomo ni haki ya wafanyakazi ambapo nchi tatu pekee barani Afrika ambazo katiba zao ndizo zimeruhusu mgomo nazo ni Kenya, Ghana pamoja na Afrika Kusini.
Awali, Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka (TUCTA), Makao
Makuu, Bi. Margareth Mandago alisema wafanyakazi hawawezi kutetea haki zao kama hawazijui hivyo wamedhamiria kutoa mafunzo nchi nzima ili wanapopigania masilahi yao waweze kutambua kanuni, sheria na taratibu za kupata haki hizo

No comments:

Post a Comment