Na Mohammed
Mhina,
wa Jeshi la Polisi
WILAYA ya Handeni m k o a n i T a n g a
, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi katika shule
zake za sekondari wilayani humo.
Ofisa Elimu shule ya Sekondari wilayani Handeni, Simon Mdaki
alisema wilaya hiyo yenye jumla ya shule 31 za Sekondari zikiwemo 29 za
Serikali na mbili za binafsi, ina walimu 58 tu wa masomo ya sayansi wakati
ambapo mahitaji ni walimu 158 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 100.
Alisema kati ya walimu 125 wa sekondari waliopelekwa Handeni mwaka
huu kufundisha katika shule mbalimbali wilayani humo, ni walimu saba tu wenye
fani ya masomo ya sayansi jambo ambalo alisema bado ni kikwazo kwa somo hilo
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mdaki alisema kuwa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi wilayani
Handeni, umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ufaulu wa wanafunzi kwa somo
hilo katika mitihani yao ya taifa mwaka jana.
Alisema ni asilimia 30 tu ya wanafunzi wa kidato cha nne
waliofanya vizuri katika somo hilo mwaka jana ambapo asilimia 70 kati yao
walifeli jambo ambalo limeleta changamoto kubwa na kuifanya wilaya hiyo
kujipanga upya kukabiliana na hali hiyo ili kuongeza kiwango cha ufaulu baadaye
mwaka huu.
Alitaja
tatizo lingine linalozikabili shule nyingi za Sekondari wilayani humo kuwa ni
ukosefu wa vyumba na vifaa vya maabara kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia mambo
kwa vitendo badala ya nadharia pekee.
Naye Mkuu
wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu akizungumzia tatizo hilo alisema kuwa
Serikali imepeleka maabara ya sayansi inayojongea (Mobile Laboratory) katika
shule nne za sekondari zenye walimu wa Sayansi.
Rweyemamu
alizitaja shule hizo zenye maabara inayojongea kuwa ni Kwamsisi, Kang'anta,
Kwankonje na Ndolwa, maabara ambazo zitawawezesha pia wanafunzi wa shule jirani
kusoma kwa vitendo masomo ya sayansi wakati serikali ikiendelea na hatua
zingine za kumaliza tatizo hilo.
Alisema kwa
kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri, Wilaya ya Handeni imeanzisha utaratibu
wa kujenga maabara ya sayansi katika shule za Sekondari Chogo iliyopo tarafa ya
Mkumburu na katika sekondari ya Mazingara iliyopo tarafani humo.
Lakini pia alisema kuwa kuna fedha za Mpango wa Maendeleo ya Elimu
ya Sekondari MMES II ambazo sasa zinatumika kujenga maabara katika shule ya
Sekondari Sindeni iliyopo katika tarafa ya Sindeni na Kisaza iliyopo katika
Tarafa ya Mzundu wilani humo ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika baadaye mwaka
huu
No comments:
Post a Comment