12 July 2013

MOAT HAIKUSHIRIKISHWA ONGEZEKO LA KODI KWA SIMU


 Na Mwandishi Wetu
MCHAKATO wa kupitisha ongezeko la kodi ya sh. 1,000 kwa kila mtumiaji wa simu kwa mwezi uliotokana na mabadiliko ya muswada wa fedha wa mwaka 2013 na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukushirikisha Chama cha Makampuni ya Simu za Mkononi (MOAT).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na MOAT jana Dar es Salaam, imeeleza kuwa chama hicho kilikutana na Kamati ya Bajeti ya Bunge ili kupata usahihi wa maana ya huduma za mawasiliano ya simu kama ilivyoainishwa katika muswada wa mwaka 2013.

Imesema katika kikao hicho, mawasiliano ya simu yalitafsiriwa kuwa ni huduma yoyote inayotolewa na kampuni ya mawasiliano ya simu kwa kutuma, kupokea mawimbi, maneno, picha na sauti au habari ya aina yoyote kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa picha au mfumo mwingine wowote.
“Sisi kama waendeshaji wa mitandao ya simu hatukushirikishwa katika kujadili mfumo huu mpya wa kulipa kodi ya sh.1,000 kwa kila laini.Tunaiomba serikali iliangalie upya suala hili la ushuru huo ambapo kwa kufanya hivyo watawezesha ukuaji wa mawasiliano ya simu nchini Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Ukuaji wa mawasiliano ya simu nchini Tanzania unaridhisha ambapo takwimu zinaonesha ukuaji huo ni asilimia 48, kiasi ambacho ni sawa na watu takriban milioni 22 ambapo kati yao watu milioni 8 hutumia chini ya sh.1,000 kwa mwezi kwa mawasiliano ya simu.
Taarifa hiyo ya MOAT imeeleza kuwa inatambua jitihada za serikali katika kukusanya kodi kwa ajili ya mipango ya maendeleo kwa wananchi, Hata hivyo MOAT imebainisha kuwa kuanzishwa kwa kodi hiyo kunakinzana na juhudi za kuwapunguzia mizigo ya kodi wananchi wenye kipato cha chini.
Imesema kuwa ukuaji wa mawasiliano ya simu katika muongo ujao utatoka maeneo ya vijijini, hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza kwamba uanzishwaji wa kodi mpya ya sh. 1, 000 kwa kila mtumiaji wa simu kila mwezi utazuia juhudi zaidi za ukuaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini kwa sababu watu wengi ambao ni wenye kipato cha chini hawataweza kutumia mawasiliano ya huduma hiyo.
"Ulipaji wa kodi mpya ya sh.1,000 kwa kila mtumiaji wa simu kwa mwezi utadhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano ya simu hadi hivi leo, ambapo tumeshuhudia huduma hiyo imezidi kuwa nafuu kwa ajili ya wote," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment