25 July 2013

SITTA AZITAKA SERIKALI TATU

  • AHAMASISHA MAANDAMANO KUPINGA VIONGOZI MAFISADI
  • HARAMBEE ZA MAMILIONI YA FEDHA KILA WIKI ZAMTISHA


 Na Waandishi Wetu

WA Z I R I w a A f r i k a Mashariki, Samuel Sitta, ameunga mkono Tanzania kuwa na mfumo wa Serikali tatu lakini sio marais watatu na kwamba wanaopigania jambo hilo wanataka kugombania madaraka.Sitta alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa majadiliano ya Rasimu ya Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Vijana la Katiba nchini.


Alisema mfumo wa kuwa na marais watatu utaongeza gharama, hivyo ni vyema ziwepo Serikali tatu ambazo zitaongozwa na rais mmoja. Alisema fedha ambazo zingetumika kuhudumia Serikali yenye marais watatu zitatumika kwenye sekta za afya, elimu na kilimo."Leo tukiwa na marais watatu, mmoja aende China, mwingine Uingereza sijui wapi sasa hizo gharama zitatoka wapi?"Alihoji.

Ubinafsi wa viongozi

Katika hatua nyingine, Waziri Sitta amewataka Watanzania kuandamana kupinga viongozi walafi na wabinafsi wanaotaka kujilimbikizia mali.Alisema kwa hata Tanzania iwe na Katiba nzuri namna gani bila wananchi kupigania maadili ikiwa ni pamoja na kuandamana kupinga viongozi wa aina hiyo.

"Katika nchi yetu tumekuwa na viongozi wengi wa kijamii ambao ni walafi sana na wabinafsi, kama vijana hamtakuwa mstari wa mbele kuwapinga basi nchi yetu haitatawalika,"alisema, Sitta.Akifafanua zaidi alisema haiwezekani baadhi ya watu wachache wawe matajiri wakubwa huku wananchi wengi wakiwa masikini kupitiliza. "Kama ni suala la akili watu wote wanazo akili, inakuwaje wao tu ndio wawe matajiri?" Alihoji.

Alisema ni vema katiba mpya ielekeze utungaji wa sheria zitakazozuia ubinafsi, udikteta, ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kuzuia kiongozi kufanya kazi kwa masilahi yake binafsi.Alifafanua zaidi akisema ili nchi ipate maendeleo, Serikali inatakiwa kupunguza fedha katika utawala na kuzielekeza katika miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Alisema kuna baadhi ya viongozi (bila kuwataja) wameanzisha kampuni hewa kwa lengo la kujipatia fedha, lakini uchunguzi unafanyika dhidi yao bila matokeo kutangazwa.Alihoji uchunguzi wa aina hiyo utafanyika hadi lini? "Kumebainika kuwa kuna kampuni tatu hewa ambazo zinajipatia fedha kwa njia isiyo halali, uchunguzi unafanyika ili kutafuta ukweli, japokuwa hatuambiwi matokeo ya uchunguzi mara baada ya kukamilika, nchi yetu itaendelea kuwa ya uchunguzi hadi lini?"Alihoji Bw.Sitta.

Katika hatua nyingine, Sitta amewashangaa baadhi ya viongozi nchini wanaohifadhi fedha zao nchi za nje na kuhoji lengo lao ni nini?Alisema siku hizi vyombo vya habari vinafanya kazi nzuri ya kuwafichua viongozi wabadhirifu h i v y o k u s a i d i a wa n a n c h i kuwafahamu.

Harambee makanisa

Waziri Sitta alipoulizwa na waandishi wa habari maoni yake kuhusiana na watu wanaotoa misaada makanisani, alijibu kuwa hata yeye kipindi cha nyuma aliwahi kusimamia kujenga msikiti wilayani Mirambo, lakini haikuwa shida.

"Lakini kwa sasa viwango vinatisha mtu anachangisha mamilioni ya fedha kila wiki...hii inatisha," alisema na kuhoji kuwa watu hao fedha wanazipata wapi? Alisema kuwa inawezekana nyuma yao kuna watu wanaowasaidia.

Mrema anena

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Augustino Mrema, alisema mfumo wa Serikali tatu gharama kubwa kiuendeshaji na utasababisha migogoro nchini.Akizungumza na Majira, Mrema alisema kuwa Serikali tatu zinafaa kinadharia na sio kiutekelezaji kwani zitaweza kuhitaji gharama kubwa katika uendeshwaji wake.

“Maoni yangu binafsi juu ya rasimu mpya ya uundwaji wa Katiba Mpya, kuwa Serikali tatu inafaa kinadharia na sio kiutekelezaji, mfano kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zanzibar nani atagharamia hizo Serikali?" Alihoji.

Aliendelea kuhoji; " Huku kuwe na mabunge matatu na la muungano, pia kuwe na Ikulu ya muungano, Ikulu ya Tanzania na Zanzibar, nani atakayeweza kugharamia Serikali zote tatu‚“ alihoji Mrema.

Imeandikwa na Kassim Mahege, Frank Monyo Penina Malundo na Neema Malley


 

3 comments:

  1. Serikali tatu ndio suluhisho la matatizo ya muungano na haiepukiki,kama tatizo ni maraisi watatu basi serikali ya zanzibar na ile ya Tanganyika zipewe uhuru wakutoa jina wanalotaka kumwita kiongozi wa serikali zao,Sisi Znz tutatumia Raisi na Tanganyika wataamua wenyewe,wkimwita gavana,au W mkuu,au chifu sawa tuu.suala la gharama halina msingi wowote kwani sasa hivi Rais wa zanzibar anahudumiwa nanani? Tanganyika itabeba gharama zake zenyewe kama ambavyo zanzibar inabeba gharama zake,watanganyika mnawasiwas wanini na mnarasilimali kibao.

    ReplyDelete
  2. Serikali tatu hapana, ni gharama kubwa.Labda kulinda Muungano kwa gharama yoyote.

    ReplyDelete
  3. Serikali Tatu serikali mbili vyote ni ushenzi tu kama kweli tunajivunia mshikamano basi serikali ya zanziba ivunjwe tuwe na serikali moja tu ya muungano wa Tz.

    ReplyDelete