25 July 2013

HATARI TUPU



Na Mwandishi wetu
UJENZI wa majengo marefu jijini Dar es Salaam unazidi kuleta hofu baada ya kubainika jengo la ghorofa zaidi ya saba lenye nyufa kiasi cha kutishia maisha ya wanaolitumia na wapitanjia.Uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini kuwa jengo hilo lipo mtaa wa Asia na Mali karibu na kituo cha mafuta Barabara ya Samora jijini Dar es Salaam. Jengo hilo lina nyufa nyingi kiasi cha kutishia wapita njia na baadhi ya watumiaji wake.

Mmiliki wa jengo hilo alipotakiwa kutolea ufafanuzi hali hiyo na sababu ya kuruhusu liendelee kutumika alijibu kuwa; "Kama unataka kuandika habari kuhusu ufa kuna majengo zaidi ya 10 ambayo yana nyufa hapa Dar es Salaam kama upo tayari nikupeleke ili nikuoneshe hayo majengo na ukitaka kuandika uanze na hayo," alisema.
Alisema kila baada ya siku wakaguzi kutoka manispaa ya Ilala hufika katika jengo hilo kulikagua, hivyo majibu yote yanapatikana manispaa hiyo."Mimi sina jibu la kukwambia zaidi ya wewe uende manispaa ndio watakupa majibu yote unayotaka... sawa?"Alisema mmiliki wa jengo hilo.
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni iliyojenga jengo hilo (jina tunalo) alisema jengo hilo lilianza kujengwa mwaka 2006 na kukamilika 2008 hivyo lina miaka zaidi ya sita sasa.Alisema kama lingekuwa na matatizo basi wasingepewa vibali vya kuruhusu kutumika. Alisema tangu lilipoanza kujengwa lilikuwa linakaguliwa na mamlaka husika hadi lilipomalizika kujengwa, kwani lina vibali vyote na ndio maana watu wanalitumia.
"Ukitaka kufuatilia basi lazima uende kwenye mamlaka husika utapata hicho unachokitafuta," alisema ofisa huyo. Baadhi ya wapangaji katika jengo hilo walisema wao wamekuwa wakimuona mmiliki wa jengo hilo na mhandisi wa kampuni iliyolijenga wakifika katika jengo hilo mara kwa mara na kulikagua, lakini hawaelewi ni kwa nini wanafanya hivyo.
"Huwa tunawaona mmiliki wa jengo hili na injinia ambaye amelijenga jengo hilo mara kwa mara wanakuja mbele ya jengo na kisha kuelekezana kuelekea juu kwa kuwa hatuelewi basi huwa tunawaangalia tu, lakini kumbe kuna ufa sasa ndio tumejua ni kwa nini wanafanya hivyo," alisema mmoja wa wapangaji na kuongeza kuwa kipindi cha milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi Mbagala, jengo hili lilitikisika sana hadi wakaamriwa wafunge maduka watoke.Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala ili kuzungumzia suala hilo zilishindikana kwa kile kilichoelezwa na Katibu Muhutasi wake kwamba ana siku maalum ya kumuona.
Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alijibu kwamba yupo kwenye kikao, hivyo atume ujumbe mfupi wa simu. Pamoja na kutumiwa ujumbe huo tangu Jumatatu na gazeti hili kuzidi kumfuatilia, alijibu suala hilo atampa injinia wa manispaa ya Ilala afuatilie.
P amo j a n a a h a d i h i y o alipofuatiliwa zaidi aliahidi kutoa namba za simu za injinia huyo kwa mwandishi wa gazeti hili ili awasiliane naye, lakini hakufanya hivyo na alipopigiwa simu ilikuwa haipokelewi.Gazeti hili pia lilimtafuta Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Injinia Steven Mlote, ambapo alisema kwamba yuko mkoani Arusha, lakini amewaagiza baadhi ya wafanyakazi kufuatilia jengo hilo mara moja.
Alipotafutwa tena ili atoe ufafanuzi kuhusu jambo hilo, Mlote alisema alikuwa hajapata taarifa zozote kutoka kwa wasaidizi wake, hivyo alimtaka mwandishi wa habari hii kufika ofisini kwake ili akapate taarifa.
Licha ya mwandishi kufika ofisi za ERB hakupata ushirikiano wowote na Mlote alipotafutwa tena simu yake haikupatikana.
Kwa upande wa Ofisa Uhusiano wa Wakala wa Majengo (TBA), aliyejulikana kwa jina moja la Mariam alipotakiwa kuzungumzia jengo hilo, alitaka aandikiwe maswali ili ayajibu kimaandishi

No comments:

Post a Comment